Mfumo wa Tiketi Mtandao Kuanza kutumika Aprili, 2022

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu Kielektoniki (NIDC), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) na wadau wengine tarehe 28 Machi, 2022 wamefanya semina ya kuwajengea uelewa Wahariri wa habari nchini kuhusu mfumo wa Taketi Mtandao.

Semina hiyo iliyofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ilifungulia na muwakilishi wa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Swalehe Byarugaba ambapo wahariri wa habari na waandishi walipata kujifunza masuala mbalimbali kuhusu mfumo wa Taketi Mtandao unaowezesha abiria kukata tiketi za mabasi popote alipo kielekroniki. Bw. Byarugaba alisema kuwa mfumo huo utaanza kutumika kwa majaribio kukata tiketi za mabasi ya masafa marefu kwa miezi mitatu kuanzia tarehe moja Aprili, 2022 hadi tarehe 30 Juni, 2022 ambapo katika kipindi hicho LATRA na TRA hazitamuadhibu msafirishaji yeyote kuhusiana na matumizi ya mfumo huu, baada ya kipindi hicho mfumo huo utaendelea kutumika rasmi.

Bw. Byarugaba alieleza faida mbalimbali za mfumo wa Taketi Mtandao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa za abiria na mauzo ya tiketi, kuzua uvujaji wa mapato ya wasafirishaji na Serikali.

Aliongeza kuwa, TRA, LATRA na NIDC wataendelea kutoa elimu ya mfumo huo kwa wadau na umuhimu wa kulipa kodi kwa uhiari.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Uchukuzi Bw. Gabriel Migire alisema kuwa Mfumo wa Tiketi Mtandao umeleta utatuzi wa changamoto mbalimbali katika usafiri wa abiria kwa mabasi ya masafa marefu zikiwemo changamoto za abiria kubugudhiwa, kupandishiwa nauli kiholela na kulazimika kusafiri kwa basi ambalo hakulichagua.

Aliongeza kuwa, wamiliki wa mabasi walikuwa wakilalamikia kulazimika kuwalipa wapiga debe kwa mapato ya uuzaji tiketi na kuwa Wizara umedhamiria kusimamia mfumo huo utanaowezesha abiria kupata haki zake na wasafirishaji kupata haki zao.

“Wizara iliandaa kanuni za kusimamia mfumo wa utoaji leseni za kielektroniki, tunaamini kuwa, kufikia tarehe moja Julai, 2022 wadau wote watakuwa wamepata uelewa wa kutosha kuhusu mfumo huo na changamoto husika zitakuwa zimefanyiwa kazi. Baada ya kipindi cha majaribio atakayekiuka kanuni hizo atawajibika kupata adhabu kwa kosa alilofanya” Alisema Bw. Migire