Mnamo tarehe 19 Juni, 2023 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilisitisha ratiba ya mabasi ya Ally’s Star na Katarama Luxury kuanza safari saa tisa (9:00) alfajiri na saa kumi na moja (11:00) alfajiri na kupewa ratiba ya kuanza safari saa kumi na mbili (12:00) asubuhi. Hatua hiyo ilitokana na Mamlaka kupata taarifa na kuthibitisha uwepo wa mabasi ya kampuni hizo yanayokwenda mikoani kuchezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (Vehicle Tracking System - VTS) hivyo kusababisha kusafiri kwa mwendo kasi kwa lengo la kufanya mashindano ya kuwahi kufika kwenye vituo/stendi za mabasi.
Hivyo Mamlaka kwa kuzingatia jukumu lake la kukuza usalama katika sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma haiwezi kuacha matendo haya hatari yenye kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao bila kuchukua hatua stahiki.