Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ni Mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019. Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). LATRA imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususan usafiri wa mizigo na abiria (mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu) usafiri wa reli na usafiri wa waya. Makao Makuu ya LATRA yapo Dodoma na Mamlaka ina ofisi katika mikoa yote ishirini na sita (26) ya Tanzania Bara.
Usafiri ni huduma ya lazima na kiashiria muhimu cha maendeleo katika jamii yoyote. Maendeleo katika huduma za usafiri yanaakisi mabadiliko katika mtindo wa maisha, ustaarabu na maendeleo ya kiuchumi.
Katika zama hizi, matumizi ya teknolojia ya kisasa yanaleta mapinduzi katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya usafiri ardhini, LATRA inawezesha matumizi ya teknolojia hizo kama suluhisho kwa changamoto katika sekta ya usafiri. Hii inafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi. Moja ya mafanikio yanayotambuliwa ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS). Mfumo huu umekuwa ukifanya kazi tangu mwaka 2017 na umeonesha matokeo chanya katika kuokoa maisha na mali. LATRA itaendelea kutumia teknolojia kutatua changamoto za usafiri nchini.