Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeandaa maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu wa Ardhini 2025 inayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 24 hadi 29, 2025. Wiki hii itaadhimishwa Nchini Tanzania kuunganana na Nchi nyingine duniani kutambua Siku ya Usafiri Endelevu Duniani (World Sustainable Transport Day) tarehe 26 Novemba kila mwaka.
Katika Azimio Na. 77/286 la tarehe 16 May 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN General Assembly) liliazimia kila mwaka tarehe Novemba 26 iwe ni Siku ya Usafiri Endelevu Duniani (World Sustainable Transport Day) na kuzikaribisha Nchi zote duniani, Taasisi za Umoja wa Mataifa, Taasisi za Kikanda na Kimataifa, Jumuiya za Kiraia, ikijumuisha Taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs), na wadau wengine wote wa usafiri na usafirishaji, kuiadhimisha siku hii kwa kutoa elimu na kuandaa shughuli zitakazokuza elimu juu ya masuala ya usafiri na usafirishaji, hususan aina za usafiri bora na salama, kuhamasisha usafiri unaotunza mazingira, kujenga miundombinu ya usafiri inayozingatia watu wenye mahitaji maalum, na masuala mengine ya usafiri bora, salama na endelevu. Soma Zaidi