Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inautangazia umma kuwa Wiki ya Usalama wa Reli Tanzania itaadhimishwa Nchini kuanzia tarehe 10-16 Oktoba, 2022. Maadhimisho hayo yatazinduliwa rasmi na Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Tunapoadhimisha Wiki hii, tunawahimiza watumiaji wa huduma za reli na wananchi wote kwa jumla wawe makini, waangalifu na wachukue hadhari za kiusalama wakati wote wanapotumia huduma za reli wakiwa kwenye vituo vya reli, ndani ya mabehewa na hata wanapopita kwenye maeneo ya reli. Ni muhimu kufahamu kwamba treni zinakwenda kwa mwendo kasi na zinaweza kukawia au kushindwa kusimama ghafla inapotokea dharura. Hivyo basi, ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha.
LATRA ikiwa ni Mdhibiti wa Huduma za Usafiri wa Reli Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ina wajibu wa kuhakikisha kuwa huduma za usafiri wa reli hapa Nchini zinatolewa kwa ubora na usalama kwa watuamiaji na wananchi kwa jumla.