Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa siku saba kwa mabasi ya Super Feo, Abood Service na BM Coach kujirekibisha haraka kabla hawajasitishiwa leseni zao za kutoa huduma baada ya kubainika kukiuka masharti ya usafirishaji na kusababisha ajali mfulululizo.
Hayo yamebainishwa na CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA alipozungumza na waandishi wa habari Septemba 12, 2024 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
CPA Suluo amezitaka kampuni hizo kutii Sheria zilizopo ili kuendelea kuboresha utoaji huduma katika sekta ya usafiri nchini kwani kufanya hivyo kutachochea kupunguza ajali zinazotokana na uzembe na kusababisha vifo pamoja na kuharibika kwa mali.
CPA Suluo ameeleza kuwa, Mamlaka imelazimika kuwaita wamiliki na wasimamizi wa kampuni hizo ili kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kabla ya kuchukua hatua za kisheria na kampuni hizo zimeahidi kutii maelekezo waliyopewa.
“Kwa kuwa LATRA imepewa jukumu la kusimamia Sheria na Kanuni zilizopo tumewaita wamiliki wa kampuni hizo kwa ajili ya kuwasilikiliza juu ya hatua tuliyotaka kuichukuwa na wameahidi kuwa watabadilika na kutii Sheria ikiwemo hatua ya kuweka utaratibu wa madereva kuwa wawili katika kila basi ikiwa ni pamoja na kutumia kifaa cha utambuzi (I- Button)” ameeleza CPA Suluo.
Ameongeza kuwa, endapo tabia ya ukiukaji Sheria itakithiri kwa kampuni hizo Mamlaka haitosita kuchukuwa hatua ya kuwatoa katika ratiba za usiku na kuwarudisha katika ratiba za kuanzia saa 11 alfajiri na kuishia saa 6 usiku.
Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, yapo masharti saba ambayo wasafirishaji hao waliyakubali na kuyasaini kabla ya kupewa kibali cha kutoa huduma ya usafirishaji usiku na kwamba, licha ya makubaliano hayo tayari baadhi yao wameanza kuyakiuka.
Ametaja masharti hayo kuwa ni pamoja na kusaini tamko hilo la LATRA na kulikubali, kuunganisha mabasi kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Madereva kupokezana kwenye safari za zaidi ya saa nane, madereva kusajiliwa na kuthibitishwa na kupewa Kifaa cha Utambuzi (I-botton), kuwa na Ofisa mahsusi ambaye jukumu lake ni kufuatilia mabasi ya kampuni yake, kutoa taarifa sahihi za abiria wanaosafiri, mizigo kuwekwa alama ya utambulisho ya mhusika na kutoruhusu asiye abiria kupanda kwenye gari kabla na wakati wa safari.
“Baadhi ya wasafirishaji wameanza kukiuka masharti hayo na sisi kama LATRA kwa mamlaka tuliyopewa na Sheria, tunatakiwa kuwalinda Watanzania, hatuwezi kuvumilia kuona masharti haya yanakiukwa” amesema CPA Suluo.
Naye Abdallah Kiongozi, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), ameishukuru LATRA kwa kuzipa kampuni hizo nafasi ya kujirekebisha kutokana na makosa yao.
“Chama chetu hakiko tayari kumtetea msafirishaji anayekwenda kinyume na taratibu za LATRA, na niwasihi wasafirishaji kujirekebisha na kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa” amesema Bw. Kiongozi.
Kwa upande wao wamiliki wa kampuni hizo wameishukuru LATRA na wamekiri makosa yaliyojitokeza na kuahidi kujirekebisha na kutekeleza waliyoagizwa na LATRA. Na wametoa wito kwa wasafirishaji wengine kutii Sheria zilizowekwa na kuomba wananchi kuchangua muda sahihi wa kusafiri wakati wanakata tiketi ili wajue muda wa safari kuanza na wa kufika na kuepusha changamoto zozote ikiwemo kuchelewa kufika kituoni.