Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

BW. NDUHIYE: AITAKA LATRA KUSHIRIKI KIKAMILIFU MABORESHO YA SERA YA TAIFA YA USAFIRISHAJI
Imewekwa: 10 Sep, 2024
BW. NDUHIYE: AITAKA LATRA KUSHIRIKI KIKAMILIFU MABORESHO  YA SERA YA TAIFA YA USAFIRISHAJI

Bw. Ludovick Nduhiye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi ametembelea Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) jijini Dodoma Septemba 9, 2024, kwa lengo la kujifunza namna LATRA inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni.

Katika ziara hiyo Bw. Nduhiye ameongoza kikao kilichohudhuriwa na Menejimenti ya LATRA ambapo, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA na wajumbe wa Menejimenti waliwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa majukumu ya LATRA na kufafanua mikakati inayotekelezwa na Mamlaka hiyo katika kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Nduhiye amesema kuwa, amefurahishwa na jinsi LATRA inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Sera na Mipango ya Serikali na kuwa Sekta ya usafiri inapaswa kusimamiwa kwa ufanisi kwa kuwa ni sekta inayoshika uchumi wa nchi.

“Ziara yangu ni ya kujifunza na nitaendelea kujifunza, nimefurahishwa na jinsi LATRA inavyotumia mifumo ya kisasa kuboresha huduma za usafiri ardhini na inavyowafikia wadau kote nchini kwa kuendelea kufungua ofisi mpya kwa baadhi ya Wilaya na maeneo ya kimkakati nchini,” alisema Bw. Nduhiye.

Aidha ameitaka LATRA kushiriki kikamilifu katika maboresho ya Sera ya Taifa ya Usafirishaji yanayoendelea kipindi hiki ili sera mpya ihusishe masuala yanayohitajika katika kuboresha utendaji wa Mamlaka hiyo.

Mwishoni mwa ziara hiyo, CPA Suluo alimshukuru Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kuitembelea LATRA na alimkabidhi kitabu cha Sheria na Kanuni zinazotumiwa na Mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake ili kumuwezesha kufuatilia zaidi kuhusu kazi zinazotekelezwa na LATRA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo