Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CHUKUENI TAHADHARI MNAPOPITA KWENYE MIUNDOMBINU YA RELI-BANTU
Imewekwa: 10 Oct, 2022
CHUKUENI TAHADHARI MNAPOPITA KWENYE MIUNDOMBINU YA RELI-BANTU

Na Mambwana Jumbe

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw. Henry Mgalla Bantu amewataka wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya reli na kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa karibu na miundombinu ya hiyo.

Bw. Bantu amesema hayo Oktoba 10, 2022 katika hafla ya ufunguzi wa wiki ya usalama wa reli nchini iliyofanyika Dar es Salaam katika Viwanja vya Ofisi ya Reli- SGR.

Aidha, Bw. Bantu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu ya reli pamoja na kuboresha huduma zake hivyo wananchi nao wanatakiwa kuhakikisha kuwa jitihada za serikali haziendi bure kwa kuwa mstari wa mbele kuilinda miundombinu hiyo.

Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha usalama wa miundombinu ya reli na watumiaji, ni lazima kuwepo na mikakati madhubuti ya kuhakikisha jamii inapata elimu ya usalama wa reli, “Niwapongeze Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, LATRA, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) kwa hatua madhubuti wanazochukua kuendelea kuhakikisha jamii zinakuwa salama kutokana na shughuli za usafiri wa reli. Endeleeni na jitihada hizi za kutoa elimu na kuhakikisha jamii na miundombinu ya reli inakuwa salama,”ameeleza Bw. Bantu

Vilevile amesema kuwa, elimu hiyo itolewe mpaka vijijini ili kufikia watanzania walio wengi na ni vema kuwashirikisha na viongozi wa Serikali katika maeneo hayo ili kuweza kuwaeleza wananchi kuhusu usalama wa reli na usalama wao wanapopita kwenye maeneo ya reli.

Pia amesema, kazi kubwa inatakiwa kufanyika katika kubadili mitazamo ya watu kuhusu masuala ya reli kwa kuwa usalama wa reli ni wa kila mtanzania, “SGR itakapoanza hapa, treni zitakuwa zinaenda kwa mwendo kasi hivyo tusipozingatia suala la usalama tunaweza kupoteza maisha, kwahiyo usalama katika reli si jambo la kupuuza”, amefafanua Bw. Bantu

Naye Mkurugenzi Mkuu TRC Bw. Masanja Kadogosa amesema kuwa usalama wa reli ni jambo linalopewa kipaumbele katika uwezeshaji wa usafiri wa reli duniani kote na TRC wamekuwa wakifuata taratibu na kanuni za usalama zilizowekwa kwa taasisi za Kimataifa na za Kikanda kwa maana ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Sheria za hapa nchini ikiwemo Sheria ya Reli Na. 10, 2017 na kanuni zake

“Kitu cha kwanza kabisa katika reli ni usalama, tukizungumzia SGR, kosa dogo linaweza kuleta madhara makubwa   kwahiyo ni lazima tuweze kubadili mitazamo yetu kuhusu uendeshaji wa treni hizo ili kupunguza makosa ya kibinaadam yanayoweza kutokea. Tunakoelekea, tutakuwa tunaisikiliza sana LATRA kwa miongozo mtakayotupatia kwa kuwa ndio mdhibiti wa usafiri ardhini ikiwemo usafiri wa reli,”amefafanua Bw. Kadogosa.

.Wiki ya reli inaadhimishwa Oktoba kila mwaka kwa nchi wanachama wa SADC kupitia Shirikisho la Reli Kusini mwa Afrika (SARA) na Kaulimbiu ya maadhimishi hayo ni Chukua Tahadhari, Treni Zina Mwendo wa Haraka, ni Hatari na inafanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 16, 2022.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo