Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA DKT. SULUO: NAULI ZA DART NI ZA MPITO
Imewekwa: 18 Dec, 2025
CPA DKT. SULUO: NAULI ZA DART NI ZA MPITO

CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema Shilingi 1000 wanazotozwa abiria wanaotumia usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ni nauli ya mpito na nauli halisi zitatumika baada ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuwasilisha maombi ya nauli mpya.

CPA Dkt. Suluo amebainisha hayo Desemba 17, kwenye Maonesho ya Mkutano wa 18 wa Tathmini ya Utendaji kazi wa Sekta ya Uchukuzi uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kuanzia Desemba 15 hadi 17, 2025.

“Nauli ya mpito ya BRT iliridhiwa kuwa shilingi 1,000 kwa Tangazo la Serikali la Agosti 29, 2025 na hii ilikuwa inawapa uhakika wale wanaoleta mabasi kuwa nauli hii wanaweza wakaanza nayo hadi pale DART itakapoleta maombi rasmi ya mapendekezo ya nauli baada ya kukaa na watoa huduma wa usafiri huo. Kwa sasa nauli hizi zinamtosheleza mtoa huduma kutopata hasara lakini kutopata faida ili aingie sokoni na anaweza akaona faida kwa sababu abiria ni wengi, lengo la kuweka nauli hii ni kuwavutia wawekezaji wengine kutoa huduma,” amesema CPA Dkt. Suluo.

Pia CPA Dkt. Suluo ameipongeza DART kwa kutatua changamoto ambazo zilibainika hapo awali na kufanikisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, “Mamlaka ilifanya ziara ya mradi wa BRT awamu ya pili na kabla ya kutangazwa kwa nauli ya shilingi 1,000 kulikuwa na changamoto kwenye uendeshaji ambapo changamoto hiyo ilitatuliwa na huduma za usafiri zikaanza kutolewa. Tunawapongeza na kuwashukuru kwa uboreshaji wa BRT awamu ya pili kwenye mfumo wa kukusanya nauli pamoja na mabasi kuwa mengi hali iliyopelekea mabasi 60 kuazimwa kwenda BTR awamu ya kwanza,” amesema CPA Dkt. Suluo.

Kwa upande wake Bw. Said Tunda, Mtendaji Mkuu DART amesema kuwa, “Serikali inawajali sana wananchi wake ndio maana hata baada ya kuharibika miundombinu iliyosababisha changamoto ya usafiri kwa wananchi, huduma zinaendelea katika vituo vingi vya mwendokasi kwa kulipia gharama ya shilingi 1,000 tu ambapo ni ongezeko la shilingi 250 kutoka nauli ya awali,” amesema Bw. Tunda.

Aliongeza kuwa, nauli ya shilingi 1,000 inafaa kwa kuanzia kwani lengo sio kuwaumiza watumia huduma bali ni kuhakikisha abiria wanapata huduma bora na endelevu kwani wakati huduma za BRT hazipo, abiria walikuwa wanatozwa hadi shilingi 6,000 kwa safari moja walipotumia vyombo vidogo vya usafiri.

Kwa mujibu wa Kanuni za LATRA za Tozo za mwaka 2020, watoa huduma wanatakiwa kutoa matangazo ya nauli mpya kwa siku kumi na nne (14) kabla ya kuanza kutumia nauli mpya kupitia vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi.

 

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo