CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewaasa abiria wa mabasi ya masafa marefu kutumia Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi https://tiketi.latra.go.tz/ kukata tiketi zenye nauli halali zilizoidhinishwa na Serikali kupitia LATRA ili kuepuka ulanguzi wa nauli unaosababisha migogoro baina ya abiria na wasafirishaji inayotokana na malipo ya pesa taslimu.
Dkt. Suluo amebainisha hayo alipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli Desemba 6, 2025 Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha hali ya huduma za usafiri zinaimarika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Vilevile amewataka abiria kuthibitisha malipo ya tiketi zao kwa kutumia Mfumo Tumizi wa LATRA App unaopatikana kupitia Play Store na App Store kwenye Simu janja na kuwasiliana na LATRA bila malipo kwa namba 0800110019 au 0800110020 kwa changamoto yoyote wanayokutana nayo pindi wanapokata nauli za mabasi.
CPA Dkt. Suluo amefafanua kuwa, katika ukaguzi huo Mamlaka imebaini kuwepo kwa watu wanaowalaghai abiria kwa kuwaandikia tiketi za makaratasi zisizo rasmi na kuwatoza nauli kinyume na Taratibu zilizopo.
“Katika ukaguzi uliofanyika Mamlaka imebaini baadhi ya watu wamekuwa wakifanya udanganyifu kuwa ni mawakala wa ukataji tiketi za mabasi na kuwatoza nauli kinyume na Sheria, watu hao wanakuwa na tiketi hadi 30 kutoka kampuni mbalimbali za mabasi na kuziuza kwa bei isiyo elekezi huku wakiwapeleka abiria kwenye mabasi ambayo hawayafahamu,” amesema CPA Dkt. Suluo.
Pia CPA Dkt. Suluo amewasisitiza abiria kuweka taarifa zao muhimu kwenye tiketi ikiwemo, Jina la abiria, namba ya basi, tarehe na muda wa safari, kituo cha kuanzia na kumalizia safari, nauli iliyolipwa, anwani na namba za simu za msafirishaji na namba ya tiketi husika.
Naye Bi. Upendo Nestory, abiria aliyezidishiwa nauli ameishukuru Mamlaka kwa kazi nzuri inayoifanya hasa ya kutetea abiria, “Nimefurahi sana mmekuja hapa kutusaidia, kiukweli sisi wananchi tulikuwa tunanyanyasika sana, na tulikuwa hatuna budi kulipa kiasi kilichozidi kwa sababu tulikuwa hatujui nini cha kufanya na tunaitaka safari, mimi namshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wote, kwa hili la leo nimeamini kuwa wanatuona na wanatusaidia,” amesema Bi. Upendo.
Ukaguzi wa mwisho wa mwaka unaendelea mikoa yote Tanzania Bara ili kuhakikisha wasafirishaji na watoa huduma wanafuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Usafiri Ardhini huku abiria wakisafiri bila bughudha wakifurahia huduma za usafiri nchini.

