Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO AWASIHI WANAHABARI KUTUMIA VIZURI KALAMU ZAO
Imewekwa: 06 May, 2025
CPA SULUO AWASIHI WANAHABARI KUTUMIA VIZURI KALAMU ZAO

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi Wanahabari Mabalozi wa LATRA kutumia vizuri kalamu zao katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu ili kulinda amani na utulivu wa nchi.

CPA Suluo amesema hayo Mei 6, 2025 alipofungua rasmi semina kwa Wanahabari Mabalozi wa LATRA yenye lengo la kuwajengea uwezo wanahabari hao kuhusu uandishi wa habari za LATRA pamoja na kufahamu kazi na majukumu ya LATRA, iliyofanyika ukumbi wa TARI uliopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na wanahabari 40 kutoka vyombo mbalimbali vya habari pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejiment ya LATRA.

“Tunaelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi Mkuu na jamii inategemea sana kupata taarifa kutoka kwenu. Nawaomba mtoe taarifa sahihi, zenye ukweli, zisizo na ubaguzi na bila upendeleo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano”, amesema CPA Suluo.

Ameongeza kuwa, LATRA inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wanahabari hao kwa Mamlaka katika kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Mamlaka na pia amesema ni matarajio ya Mamlaka kuwa uwepo wao utawezesha kujifunza na kuufikishia umma wa watanzania taarifa sahihi kuhusu juhudi kubwa za kuboresha sekta ya Usafiri Ardhini zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia LATRA,” amesema CPA Suluo.

“Natumia fursa hii kutoa Pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wenye mafanikio mengi makubwa katika Awamu hii ya Sita. Kwa uchache niseme uongozi wa Mhe. Dkt Samia umetujengea mazingira mazuri, bora na rafiki ya kusimamia sekta ya usafiri ardhini kwa weledi na ufanisi mkubwa tukizingatia sana ushirikishwaji wa wadau wetu wote muhimu” amesema CPA Suluo.

Kwa upande wake Bi. Ikunda Erick, mwandishi wa gazeti la Habari Leo ameishukuru LATRA kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya LATRA na Wanahabari hao pamoja na kuwawezesha kushiriki katika semina ya kuwajengea uwezo na amewasihi wanahabari wenzake kuendelea kutoa taarifa za kina kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo ili wananchi wafahamu kwa kina kuhusu jitihada zinazoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia LATRA.

Semina hiyo ya siku mbili inafanyika Mei 6 na 7, 2025 ambapo miongoni mwa mada zitakazowasilishwa ni Majukumu ya LATRA katika Udhibiti Usafiri wa Barabara, Nafasi ya TEHAMA katika Kuboresha Huduma za Usafiri Ardhini, Nafasi ya Wanahabari katika Kuboresha Huduma za Usafiri Ardhini, Mafanikio ya LATRA katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Udhibiti wa Usafiri wa Reli na Usafiri wa Waya pamoja na Nafasi ya Wanahabari katika Kutekeleza Sheria za LATRA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo