
CPA Habibu Juma Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi watumishi wa Mamlaka kutoa huduma bora kwa wateja huku wakitekeleza majukumu yao kwa uweledi, uadilifu na ufanisi kwa kuzingatia Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS) ISO 9001.
CPA Suluo amesema hayo Januari 24, 2025 alipofungua rasmi Kikao cha Sita cha Baraza la Wafanyakazi la LATRA kinachofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro Crater uliopo katika Jengo la Ngorongoro Jijini Arusha kwa lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji wa maazimio ya kikao cha mwaka 2024, kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka, kujadili mipango mipya ya Mamlaka, kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka pamoja na kufahamiana na kuongeza umoja kama wanafamilia ya LATRA.
CPA Suluo ameeleza kuwa, ni wajibu wa kila mtumishi kumjali mteja kwa kumhudumia kwa furaha na kuzidi matarajio yake ili kupunguza malalamiko na hatimaye kujenga taswira chanya kwa wateja wa Mamlaka.
“Kwa sasa tupo katika mchakato wa kupata uthibitisho wa Kimataifa wa huduma tunazozitoa yaani ISO Certification, hivyo ni muhimu sisi sote tutoe huduma zetu kwa wateja kwa kiwango cha kimataifa tukiweka wazi taratibu za upatikanaji wa huduma zetu huku tukifuata kanuni na miongozo tuliyojiwekea,” ameeleza CPA Suluo.
Katika michakato ya uandaaji wa Mipango na Bajeti za Mamlaka, CPA Suluo amesisitiza suala la ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi ya mipango inayowahusu pamoja na uandaaji wa bajeti ya Vitengo au Idara zao ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na umiliki wa taarifa muhimu za uendeshaji wa taasisi kwa jumla.
Pia, amewaasa watumishi wa LATRA kufanya kazi kwa umoja, upendo na ushirikiano ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa kuwa kila mtumishi ana mchango wake katika kufikia dira ya Mamlaka.
Mawasilisho yaliyotolewa katika kikao hicho ni Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mkakati wa Utekelezaji Awamu ya Nne (NCSAPIV) 2023-2030, Uandaaji wa Mipango na Bajeti kwa Ngazi ya Taasisi, Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS) ISO 9001 pamoja na Marekebisho ya Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024.