
CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa, LATRA haipangi nauli za daraja la kifahari (VIP/VVIP/Royal Class) za mabasi ya masafa marefu na treni za kisasa (SGR) bali inapanga nauli za daraja la kawaida zinazozingatia hali za watanzania ili waweze kumudu gharama za usafiri nchini.
CPA Suluo amebainisha hayo alipowasilisha mafanikio ya LATRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Aprili 14, 2025, Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dar es Salaam.
“Jukumu la LATRA ni kuhakikisha watanzania wanazipata hizi huduma na wanazifikia kwa kuzingatia zaidi wale wenye pato la chini na la kati, Mamlaka imeruhusu wasafirishaji kujipangia nauli za daraja la biashara (Business Class) na madaraja mengine ya juu (Royal Class) kwa kuwa eneo hili ni kwa abiria wenye uwezo kifedha na wanaoweza kufikia huduma hii ili kuruhusu ushindani kwa wasafirishaji,” amesema CPA Suluo.
CPA Suluo ameongeza kuwa, LATRA imetekeleza jukumu la kisheria kwa kupanga nauli za daraja la uchumi (Economy Class) wakati wa uanzishwaji wa huduma za treni ya kisasa (SGR), jukumu hili limetekelezwa chini ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya LATRA.
“Ni jukumu letu kupanga nauli za usafiri huu na kwa daraja la kawaida na tumewazingatia Wananchi wa kawaida kwani watazimudu nauli hizi ambapo kwa treni itakayokuwa inasimama kila kituo ni shilingi 13,000 kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na shilingi 31,000 kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambapo watoto chini ya miaka minne hawatalipia gharama hizo na watoto wenye umri wa miaka minne hadi 12 watalipia nusu gharama ya nauli hizo na nauli hizi zipo katika tovuti yetu www.latra.go.tz ’’ ameeleza CPA Suluo.
Katika Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, LATRA inaendelea kushirikiana na wadau wengine wa usafiri ili kuhakikisha huduma bora na salama kwa wananchi wote na Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuboresha sekta ya usafiri kwa kuunganisha mikoa mbalimbali nchini.