
CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi abiria wanaotumia huduma za taksi mtandao kutokubali kusitisha safari kabla ya kufika mwisho wa safari kwa kuwa ni hatari kiusalama.
CPA Suluo amesema hayo alpowasilisha mafanikio ya LATRA katika Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye semina ya kuwajengea uwezo Wanahabari Mabalozi wa LATRA kuhusu uandishi wa habari za LATRA pamoja na kufahamu kazi na majukumu ya Mamlaka, Mei 7, 2025 ukumbi wa TARI uliopo Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Msikubali kusitisha safari pindi dereva wa taksi mtandao anakuomba kufanya hivyo kwa kuwa sio tu mnahatarisha usalama wenu, lakini pia mnapoteza mapato ya Serikali. Mnapokutana na changamoto hiyo, tupigieni simu bila malipo kwa namna 0800110019 au 0800110020 nasi tutashughulikia,” amesema CPA Suluo.
Vilevile amesema, Mamlaka imetoa leseni za usafirishaji kwa kampuni 26 zenye Mifumo ya Teksi/Pikipiki Mtandao ambapo hadi kufikia tarehe 07 Mei, 2025, kampuni zenye leseni hai ni 11 (42.3%), na ambao leseni zao zimeisha muda ni 15 (57.7%).
“Niwakumbushe wamiliki na watoa huduma za usafiri wa kukodi kuhakikisha kuwa wana leseni hai ya LATRA kwa kuwa ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni kutoa huduma bila leseni ya mdhibiti na watakaokiuka Sheria hiyo watawajibishwa kwa kutozwa faini kama sehemu ya adhabu,” amesema CPA Suluo.
Wakati huohuo CPA Suluo amesema, Mamlaka inawajibu wa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za usafiri na pia Mamlaka imetekeleza wajibu wa kupanga nauli za Teksi/Pikipiki Mtandao ili kulinda maslahi ya abiria, mwenye teksi/pikipiki pamoja na wenye mifumo ya teksi/pikipiki mtandao.
Kifungu cha 5(1)(g) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 kimeipa Mamlaka jukumu la kufuatilia utendaji wa sekta zinazodhibitiwa na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na salama na zenye viwango.