Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO: PUUZENI NAULI ZA SGR ZISIZOTANGAZWA NA LATRA
Imewekwa: 24 Apr, 2024
CPA SULUO: PUUZENI NAULI ZA SGR ZISIZOTANGAZWA NA LATRA

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewatoa hofu wananchi na amewaasa kupuuza taarifa za nauli za usafiri wa reli ya Kisasa (SGR) zinazosambaa mtandaoni kwa kuwa hazijatolewa na Mamlaka.

CPA Suluo amesema hayo Aprili 24, 2024 ofisini kwake mara baada ya kuona taarifa hizo mitandaoni na ameeleza kuwa hizo ni nauli za awali zinazopendekezwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kuanza kutumika katika usafiri wa reli ya Kisasa (SGR)

“Sisi ni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, ni jukumu letu kupanga nauli baada ya kupata maombi kutoka TRC, napenda niwatoe hofu watanzania kuwa wanaosambaza taarifa hizo hatujajua nia yao ni nini, kwanza sio taarifa sahihi na niwahakikishie watanzania kwamba Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inawajali watanzania wa aina zote na hasa wale wa hali ya chini, haitoweza kupanga nauli hizi zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii, hivyo tunaomba ipuuzwe,” amesisitiza CPA Suluo.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutoa nauli, LATRA ina jukumu kubwa la kutoa ithibati ya miundombinu ya reli itakayotumika, pia kutoa ithibati ya mabehewa yatakayokuwa yanabeba abiria.

“Kabla ya kutangaza nauli, lazima tutoe ithibati ya kuaza kutumika kwa njia ya reli na mabehewa. Sio muda mrefu tunatangaza, majaribio yanaendelea na kwa sasa hivi abiria wanaosafiri ni kwa ajili ya majaribio tu, hakuna nauli inayotozwa mpaka Mamlaka itangaze, kwa hiyo ipuuzeni taarifa hiyo na kila mtu aendelee na shughuli zake na hatujui waliotangaza taarifa hiyo wana nia gani,” amesema CPA Suluo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo