Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO: TUNAWEZA KUACHANA NA NISHATI HATARISHI KWA MAZINGIRA
Imewekwa: 03 Dec, 2022
CPA SULUO: TUNAWEZA KUACHANA NA NISHATI HATARISHI KWA MAZINGIRA

Na Mambwana Jumbe

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amesema ni muhimu nchi za Afrika kufikiria matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira katika shughuli za usafirishaji ikiwemo usafiri wa reli.

CPA Suluo ameyasema hayo Desemba 2, 2022 wakati akifunga rasmi mafunzo ya siku tano kwa wataalamu zaidi ya 40 wa usafiri wa reli kutoka nchi 15 za Afrika yaliyofanyika Chuo cha Utumishi wa Umma - Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa LATRA na Chuo Kikuu cha Birmingham cha nchini Uingereza.

“Ukiangalia sehemu kubwa sana ya matumizi ya reli ‘Diesel’ inatumika, kwa wenzetu mfano Uingereza wana mpango kuwa ifikapo mwaka 2040 wawe wameachana kabisa na matumizi ya ‘Diesel.’ Hivyo kupitia mafunzo haya tumepata kufahamu kuwa inawezekana kabisa kuachana na nishati ambayo si rafiki kwa mazingira katika usafiri wa reli hivyo nchi za Afrika zinatakiwa kujipanga vizuri kwani usafiri wa reli unaziunganisha nchi nyingi za Afrika” amesema CPA Suluo.

Akiyazungumzia mafunzo hayo Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Reli kutoka LATRA Mhandisi Hanya Mbawala kama mmoja ya waliopata mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo yameongeza uwanda wa kufikiria nishati mbadala itakayotumika katika uendeshaji wa treni.

“Tumeangalia kuna umuhimu wa  kutoka kwenye nishati ya ‘Diesel’ na Umeme ambayo ndio inatumika kwa sasa na kuhamia kwenye nishati mbadala ya ‘Hydrogen’ ambayo itakuwa rafiki zaidi na kufanya usafiri wa reli kuwa bora na salama. Hii ni nishati mpya kabisa na maandalizi yake yameshaanza na sisi Tanzania tumechaguliwa kuwa sehemu ya majaribio ya nishati hii” amesema Mhandisi Mbawala.

Akizungumzia faida alizozipata kutoka kwenye mafunzo haya Bw. Joseph Michael Afisa Mfawidhi wa LATRA mkoa wa Manyara, amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa fursa ili kuendana na nishati ambayo ni rafiki kwa mazingira.

“Tumejengewa maarifa makubwa ya njia ambazo tutatumia nishati rafiki kwa mazingira, mfano matumizi ya nishati ya ‘hydrogen’ na umeme ambao kwa kiasi kikubwa hauchafui mazingira. Pamoja na hayo tumeweza kujadili mikakati ambayo tutaitumia ili kushawishi serikali zetu kuanza kutumia nishati mbadala ambayo ni salama na rafiki kwa mazingira” amesema Bw. Michael.

Mafunzo hayo yamekuja wakati dunia ikikabiliana na janga la mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yametokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo usafirishaji ambapo vyombo vya usafiri vitumiavyo nishati ya mafuta hutoa hewa ya ukaa ambayo huchangia kuathiri tabaka la ‘Ozon’.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo