Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa Taasisi za Wizara ya Uchukuzi zilizofanya vizuri kiutendaji kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema tuzo hiyo ni chachu ya kuwahudumia zaidi watanzania kwa kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.
Tuzo hiyo imetolewa na Mhe. Joseph Mkude, Mkuu wa Wilaya ya Arusha aliyemuwakilisha Mgeni Rasmi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi na kupokelewa na Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA katika kilele cha Mkutano wa 18 wa Mwaka wa Tathmini ya Utendaji kazi wa Sekta ya Uchukuzi, Desemba 17, 2025 Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
CPA Dkt. Suluo amesema kuwa, hivi karibuni Mamlaka imepata ithibati ya kimataifa ya ubora wa huduma (ISO 9001) na hivyo itaendelea kuboresha huduma zake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri ardhini, kuwawezesha wasafirishaji na watoa huduma kutekeleza majukumu yao kwa uhuru bila kuwakwaza.
Vilevile amesema kuwa, Mamlaka inapaswa kuutunza ushindi huo, “Tumekuwa washindi wa kwanza kwa mara nyingine tumeendelea kutunza nafasi yetu ya ushindi na hii ni kwa namna ambavyo tumejipanga, tunajituma, tunashirikiana na pia tunashirikisha wadau katika uamuzi tunaofanya tunapotekeleza majukumu yetu ili kuacha nyuso za tabasamu kwa watanzania haswa katika sekta hii ya usafiri ardhini,” ameeleza CPA Dkt. Suluo.
Ameongeza kuwa, tuzo hiyo ni ishara kuwa LATRA inatekeleza maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutafsiri maono yake kwa vitendo kwa kutekeleza kazi na majukumu kwa ufanisi kwa watanzania ambao ni watumiaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.
Vilevile ameishukuru Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi na uongozi mzima wa Wizara, pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA inayoongozwa na Prof. Ahmed Mohamed Ame. Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwa kuisimamia Menejimenti na wafanyakazi wote wa Mamlaka na kuhakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa uweledi na ufanisi.
Tuzo hiyo ya utendaji kazi bora kwa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Uchukuzi ni muendelezo wa ushindi kwa Mamlaka ambapo LATRA imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2022/23, 2023/24, na kwa mwaka huu wa fedha 2024/25.

