Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DCP KAHATANO AFAFANUA UPOTOSHAJI KUHUSU TOZO, UDHIBITI WA PIKIPIKI NA MABASI YA SHULE
Imewekwa: 09 May, 2024
DCP KAHATANO AFAFANUA UPOTOSHAJI KUHUSU TOZO, UDHIBITI WA PIKIPIKI NA MABASI YA SHULE

Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) DCP Johansen Kahatano ametoa ufafanuzi wa taarifa za upotoshaji zinazosambaa mitandaoni kuhusu ulipaji wa tozo kwa mabasi ya masafa marefu, udhibiti wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda), magurudumu matatu (bajaji), pamoja na mabasi ya shule.  

Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam Mei 08, 2024, DCP Kahatano amesema kuwa, Mamlaka inadhibiti bodaboda na bajaji, kwa kutumia Kanuni za Vyombo vya Kukodi za mwaka 2020 iliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali Namba 78, ambapo Mamlaka inatoza ada ya TZS. 15, 000/= kwa bodaboda na TZS. 2,000/= ni gharama za maombi kwa hiyo jumla inakuwa TZS. 17, 000/= na bajaji ada yake ni TZS. 20,000/= na gharama za maombi ni TZS. 2,000/= na jumla inakuwa TZS. 22,000/=. “Viwango hivi vilipunguzwa mwaka 2020, kabla ya hapo ada ya bodaboda ilikuwa TZS. 20,000/= badala ya TZS. 15,000/= ya sasa na bajaji ilikuwa TZS. 30,000/= badala ya TZS. 20,000/= ya sasa.”

Vilevile amesema Kanuni hizo ilifanyiwa marejeo mwaka 2023 kwa ajili ya kuruhusu mawakala kutoa leseni, kabla ya hapo Mamlaka ilikuwa ikifanya kazi na Halmashauri ambapo waliingia mkataba wa makubaliano na walikuwa wakipanga vituo na kutoa leseni. Kwa sasa Mamlaka imeongeza wigo na inataka huduma hizo zitolewe na mawakala ambao wanaweza kuwa ni Taasisi za Serikali, Vyama vya Ushirika, Makampuni Binafsi au Mtu Binafsi.

Aidha, kwenye udhibiti wa mabasi ya masafa marefu, DCP Kahatano amefafanua kuwa, Mamlaka inatekeleza kwa mujibu wa Kanuni za Leseni za Usafirishaji ya Mabasi ya Abiria ya mwaka 2020 na moja ya mashari ya Kanuni hizo ni watoa huduma kutakiwa kulipa levi. “Hii inatokana na kifungu cha 35 cha Sheria ya LATRA inayomtaka mtoa huduma kulipa walau asilimia 1 ya mapato ghafi kwa ajili ya levi, suala hili imefafanuliwa zaidi katika Kanuni za Tozo zilizoweka kiwango ch levi cha asilimia 0.5 na utaratibu wa kulipa levi upo kwa wadhibiti wote.”

Vilevile DCP Kahatano, ameelezea udhibiti wa mabasi ya shule na amesema kuwa Mamlaka inatoa leseni za mabasi hayo na imeainisha mapungufu yaliyopo kwenye eneo hilo na iliwasilisha mapendekezo yao kwa Shirika la Viwango (TBS) ya kuandaa viwango vya mabasi hayo na mchakato huo unaendelea.

“Wakati tunasubiri viwango, tupo wenye mchakato wa kurekebisha Kanuni zetu kwa kuweka hitaji la mabasi ya shule kukaguliwa mara mbili kwa mwaka ili tuwe na uhakika kuwa watoto wetu wanasafirishwa kwenye mabasi ambayo ni salama. Bado tunaendelea na ufuatiliaji wa kawaida wa mabasi haya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha kuwa mabasi yanakuwa katika hali nzuri. Tunaamini huko mbeleni tutakuwa na mabasi yenye viwango na salama zaidi kwa watoto wetu ikiwemo kuwa na camera ndani ya mabasi ili kuona yale yanayoendelea ndani ya mabasi hayo na tunakaribisha maoni ya wadau ya kuboresha eneo hili,” amesisitiza DCP Kahatano

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo