Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DKT. NCHEMBA ATUNUKU TUZO ZA WATOA HUDUMA BORA NA SALAMA ZA USAFIRI ARDHINI
Imewekwa: 26 Nov, 2025
DKT. NCHEMBA ATUNUKU TUZO ZA WATOA HUDUMA BORA NA SALAMA ZA USAFIRI ARDHINI

Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewatunuku wadau wa usafirishaji tuzo ya utoaji huduma bora na salama zilizoshindanishwa kuanzia Juni 2024 hadi Julai 2025 kwa lengo la kutambua na kuthamini michango ya wadau hao katika sekta ya Uchukuzi.

Dkt. Nchemba amekabidhi tuzo hizo kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, 2025 iliyoandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kufanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam Novemba 26, 2025 ambapo alikuwa mgeni rasmi wa Maadhimisho hayo.

Akizungumza mbele ya Mhe. Dkt. Nchemba, CPA Dkt. Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeipa LATRA wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa. Ameeleza kuwa, utoaji wa tuzo za Wasafirishaji Bora na Salama, ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu huo ambapo wameshindanisha watoa huduma kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2025.

Vigezo vilivyotumika kuwapata washindi kwa mujibu wa Sheria na kanuni ni pamoja na usimamizi wa vyombo vya usafiri pamoja na wafanyakazi, Ubunifu na matumizi ya teknolojia, Usalama na huduma bora kwa wateja, Matumizi ya madereva waliothibitishwa na wahudumu waliosajiliwa na LATRA, Utunzaji wa mazingira, ulipaji wa tozo za LATRA kwa wakati sahihi na uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za Usafirishaji, Bima na Usalama Barabarani,” amesema CPA Dkt. Suluo.

Pia CPA Dkt. Suluo amesema upatikanaji wa washindi hao umehusisha zoezi la mchunjo kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza washindani walichujwa kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa na awamu ya pili ilihusisha kura zilizopigwa na watumia huduma za usafiri ardhini.

Jumla ya makundi saba yametunukiwa tuzo hizo ambao ni wasafirishaji kwa magari ya mizigo ndani ya nchi na nje ya nchi, Wasafirishaji kwa mabasi ya masafa marefu (Mkoa na mkoa na nchi jirani), Madereva wa Mabasi ya masafa marefu (Mkoa na mkoa na nchi jirani), Wahudumu wa Mabasi ya masafa marefu (Mkoa na mkoa na nchi jirani), Watoa huduma za mifumo ya Tiketi Mtandao (e-Tickets Vendors), Watoa huduma ya Mifumo ya Ufuatiliaji Mwenendo wa Magari (VTS) na Watoa huduma ya mifumo ya Teksi mtandao (Ride Hailing Platforms) inayojumuisha  jumla ya washindi 27.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo