Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DKT. NCHEMBA: SEKTA YA USAFIRISHAJI NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI
Imewekwa: 15 Dec, 2025
DKT. NCHEMBA: SEKTA YA USAFIRISHAJI NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI

Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa sekta ya usafirishaji ni sekta wezeshi katika kukuza uchumi wa Tanzania na duniani kwa jumla.

Dkt Nchimbi mesema hayo alipofungua rasmi Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini Novemba 26, 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNICC) ambapo alikuwa mgeni rasmi wa Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

“Sekta ya usafirishaji ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yetu, tuitunze miundombinu ya usafiri na sote ni mashahidi kuwa miundombinu hii ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu. Hatuwezi tukapiga hatua ya maendeleo bila kuitunza, ni mali yetu sote ni chanzo kikubwa cha maendeleo ya mtu mmoja mmoja,” amesema Dkt. Nchemba.

Naye Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi amesema kuwa, shughuli zote zinazotekelezwa zinategemea sekta ya usafirishaji ambapo wananchi husafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine ili waweze kutimiza mahitaji yao muhimu na uendeshaji wa shughuli zote za kiuchumi.

Vilevile amesema, kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya usafirishaji, Wizara kwa kushirikiana na LATRA inahakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele katika shughuli za usafiri na usafirishaji nchini kupitia njia ya barabara na reli.

“Wizara itaendelea kuwakaribisha wadau wakiwemo mashirika ya maendeleo na taasisi binafsi na sekta bunifu kushirikiana na Serikali kuhakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kukuza uchumi,” amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika usafiri ardhini nchini, Tanzania inaendesha usafiri wa reli ya kisasa (SGR) kwa kutumia nishati safi ya umeme na matumizi ya nishati ya gesi kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT).

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji na yamejumuisha maonesho yaliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja na Makongamano yaliyofanyika JNICC Novemba 24 hadi 29, 2025 ambapo wadau mbalimbali walikutana kujadili na kujifunza masuala yanayohusu sekta ya usafirishaji katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo