Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAHATANO: WASILISHENI MAOMBI YA HUDUMA ZA USAFIRI WA SAA 24
Imewekwa: 18 Aug, 2023
KAHATANO: WASILISHENI MAOMBI YA HUDUMA ZA USAFIRI WA SAA 24

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa rai kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu nchini wenye nia ya kutoa huduma za usafiri kwa saa 24 kuwasilisha maombi yao ili muda wa kuanza safari hizo utakapoanza rasmi iwe rahisi kufahamu mahitaji halisi ikiwa ni pamoja na maeneo yanayotakiwa kupatiwa huduma hiyo.   

Hatua hiyo ni katika kutekeleza agizo alilolitoa Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 28, 2023 kuhusu kuanza kwa safari za usiku kwa mabasi ya masafa marefu nchini.

Hayo yamebainishwa na Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara alipozungumza na waandishi wa habari Agosti 18, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya CPA Habibu Suluo- Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Bw. Kahatano amesema kuwa, Juni 28, 2023 Serikali kupitia Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maagizo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuweka utaratibu wa mabasi kuanza kutembea saa 24 na tayari taratibu za kutekeleza maagizo zimeanza.

Wakati huohuo, Bw. Kahatano amezitaka kampuni zilizoanza kutoa huduma za usafiri kinyume na ratiba zao kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanaenda kinyume na Kanuni zilizopo, “Hivi karibuni yamejitokeza baadhi ya kampuni zinazotoa huduma nje ya ratiba ambazo wamepatiwa na wameanza safari za usiku kwenda maeneo mbalimbali jambo ambalo ni kinyume na kanuni kwa maana kila gari linatakiwa kufuata ratiba yake.”

Ameongeza kuwa, “Tumebaini kuna changamoto zimejitokeza kwa baadhi ya mabasi kuharibika usiku wa manane na mengine kuendeshwa mwendokasi kwa kuwa wanafahamu njiani hakuna udhibiti mkubwa wa askari polisi. Kwa kawaida tukibaini matukio hayo kupitia mifumo yetu, huwataarifu polisi ili wachukue hatua. Kwa kuwa muda wa usiku polisi huwa ni wachache, madereva wanatumia nafasi hiyo kufanya wanavyotaka jambo ambalo linahatarisha maisha ya abiria wanaopanda mabasi hayo.”

Vilevile Bw. Kahatano ametoa wito kwa wananchi, “Wananchi ambao wanapanga kusafiri usiku wajue kuwa huduma hizi hazijaanza rasmi hivyo wawe na subira vinginevyo watakuwa wanajaribu kuhatarisha maisha yao na wanaweza kukumbana na usumbufu pale mabasi hayo yatakapodhibitiwa njiani.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo