Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA MATUMIZI YA MIFUMO LATRA
Imewekwa: 16 Jan, 2025
KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA MATUMIZI YA MIFUMO LATRA

Mhe. Moshi Selemani Kakoso (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa jitihada za kubuni na kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayorahisisha utoaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.

Mhe. Kakoso amesema hayo kwenye kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Wizara ya Uchukuzi, LATRA na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kilichofanyika Januari 15, 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nawapongeza kwa kutumia mifumo ya TEHAMA na ninawasihi muendelee kutumia mifumo hiyo ili kuepusha rushwa na kuongeza ufanisi katika shughuli zenu za udhibiti na hii itaendelea kuleta tija na kuboresha zaidi sekta hii ya usafiri ardhini,” alisisitiza Mhe. Kakoso.

Naye DCP Johansen Kahatano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu LATRA, alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za udhibiti usafiri ardhini kwa Kamati hiyo, alisema kwa kutambua umuhimu wa TEHAMA, Mamlaka inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) uliosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za ajali nchini.

“VTS imeunganishwa kwenye vichwa vya treni na mabasi na hadi mwishoni wa mwezi Disemba, 2024 jumla ya mabasi 11,551 na vichwa vya treni 18 vilikuwa vimeunganishwa kwenye mfumo wa VTS. Kati ya vichwa hivyo, 16 ni vya Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na viwili (2) ni vya Shirika la Reli Tanzania (TRC). Kuwepo kwa mfumo huu kumeimarisha shughuli za udhibiti wa mwenendo wa udereva njiani kwa muda wote na mahali popote vyombo hivi vilipo. Pia, uwepo wa mfumo huu umesaidia udhibiti wa mwendokasi baada ya Serikali kuidhinisha mabasi kusafiri kwa masaa yote 24 hapo mwezi Oktoba 2023,” amesisitiza DCP Kahatano.

Vilevile amesema kuwa, mbali na kutambua mwenendo wa gari, LATRA imeweka teknolojia ya utambuzi wa madereva wanaoendesha mabasi muda wowote kwa kutumia kitufe cha utambuzi (i-Button) kabla ya kuanzisha safari.

Pia, DCP Kahatano ameeleza kuwa, mwaka 2023/2024, LATRA imewezesha abiria kuona mabasi yakiwa barabarani kupitia mfumo wa Taarifa kwa Abiria (Passenger Information System ama PIS) unaopatikana kwa anwani ya https://pis.latra.go.tz/   uliounganishwa na VTS ambapo abiria anaweza kufuatilia taarifa za basi analosubiri ama analosafiri nalo kwenye simu yake kupitia mfumo wa PIS ambapo ataweza kufahamu nauli, muda wa kuwasili kituoni na mwendokasi akiwa safarini.

Vilevile amebainisha mfumo mwingine kuwa ni Mfumo Jumuishi wa Tiketi Mtandao ambapo LATRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA) na sekta binafsi (wamiliki wa mabasi na watoa huduma binafsi wa tiketi mtandao) ilianza kazi ya kuunda mfumo jumuishi wa tiketi za kielektroniki kwa mabasi ya abiria mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Mfumo jumuishi utaunganishwa na mifumo binafsi ya wamiliki wa mabasi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wasafiri, kupata takwimu sahihi za watumiaji wa huduma na kuondoa changamoto ya wapigadebe kwenye vituo vya mabasi na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma,” ameeleza.

DCP Kahatano ameitaja mifumo mingine inayotumiwa na LATRA ni Mfumo wa Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva (DTS), Mfumo wa Kutoa Leseni (RRIMS) pamoja na Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA APP)

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo