Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAMATI YAIPONGEZA LATRA MFUMO WA VTS
Imewekwa: 09 Sep, 2023
KAMATI YAIPONGEZA LATRA MFUMO WA VTS

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb) pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo, wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ambao umesaidia kupunguza ajali za mabasi ya masafa marefu nchini.

Pongezi hizo zimetolewa Septemba 9, 2023 jijini Dar es Salaam ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kujionea jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.

Vilevile Mhe. Kakoso amesema kuwa, Serikali kupitia LATRA imewekeza katika mfumo huu ambao umekuwa na tija kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa suala la ajali barabarani ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla ya mfumo huo kuanza, ingawa sasa ni wakati wa kuuboresha zaidi maana teknolojia imebadilika.

Ameongeza kuwa, "Kamati imebaini kuwa LATRA wanafuatilia mfumo lakini bado kuna baadhi ya madereva na wanaofunga vifaa vya mfumo huu si waungwana kwa sababu wamekuwa wanaingilia mfumo ambapo athari zake tumekuwa tukiziona ikiwemo suala la ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania. Hapa Kamati tunaitaka LATRA ikae pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wadau wengine ili kuhakikisha kampuni hizo zinafuata Sheria, taratibu na kanuni zilizopo na kuzichukulia hatua pindi wanapozikiuka.”

Wakati huohuo Mhe. Kakoso ameipongeza LATRA kwa kubuni mifumo ya kielekroni inayorahisisha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo. “Kwanza niwapongeze sana LATRA, naamini mapinduzi makubwa ya kisayansi yaliyofanywa yakisimamiwa vizuri na serikali yanakwenda kuleta mabadiliko makubwa nchini, sambamba na hilo wasimamieni wamiliki wa magari ya masafa marefu ambao kwa mujibu wa kanuni wanatakiwa kuwa na madereva wawili ili dereva asiendeshe gari kwenye hali ya uchovu wafanye hivyo, kwa atakaekiuka asimamishiwe leseni yake ya usafirishaji au kufungiwa kabisa kwa sababu nyie ndio mna mamlaka hayo Kisheria” amesema Mhe. Kakoso.

Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati hiyo, Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) amesema kuwa Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ni wa muhimu kwani unasaidia kupunguza madhara ya ajali kwa kuepusha tabia hatarishi walizonazo madereva na hivyo kuhakikisha usalama wa basi na abiria waliopo ndani yake

“Katika ziara hii Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wamejifunza namna mfumo wa VTS unavyofanya kazi, kimsingi mfumo huu ni muhimu kwani unasaidia madereva kubadilisha tabia zao (hatarishi), madereva wanapaswa waelewe kuwa vyombo vyao vimebeba abiria hivyo usalama kwao iwe ni kitu cha kwanza,” ameongeza Mhe. Prof. Mbarawa.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kutembelea LATRA na kujifunza kuhusu shughuli za kiudhibiti huku akielezea mwelekeo wa LATRA katika kudhibiti makampuni yanayohusika na ufungaji wa vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari (VTD).

“Napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwani hii ni mara ya kwanza imetutembelea na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mfumo mzima wa VTS unavyofanya kazi pamoja na changamoto zake, kikubwa wameweza kufahamu kuwa makampuni yanayofunga vifaa hivi hayadhibitiwi moja kwa moja, hivyo hata inapotokea kuchezewa kwa mifumo mara nyingi anayeadhibiwa ni mmiliki pekee, kanuni zimeshatungwa na Mhe. Waziri Prof. Mbarawa ametueleza kuwa zipo katika hatua za mwisho hivyo hivi karibuni zitakuwa tayari na itatusaidia sana katika kutekeleza majukumu yetu,” amesema CPA. Suluo.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo