Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KANALI MAIGA: ZINGATIENI MATUMIZI YA TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 07 Dec, 2022
KANALI MAIGA: ZINGATIENI MATUMIZI YA TIKETI MTANDAO

Na Mambwana Jumbe

Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe. Kanali Hamis Maiga amewataka wasafirishaji kuzingatia matumizi ya Tiketi Mtandao na amewasihi abiria kuhakikisha wanapatiwa tiketi hizo pindi wanaposafiri.

Kanali Maiga alisema hayo Desemba 7, 2022 alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu wakati wa ukaguzi wa pamoja wa mabasi ya masafa marefu uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Jeshi la Polisi pamoja na wadau wengine wa usafirishaji katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro 

Akizungumzia faida za mfumo huo, Kanali Maiga alisema “mfumo huu una manufaa mengi, ukiachana na kuipatia Serikali mapato, unamuondolea abiria bugudha kama vile kuzidishiwa nauli kwa baadhi ya wasafirishaji ambao sio waaminifu katika kazi zao na pia unamsaidia mmiliki wa gari kupata stahiki zake kwakuwa anaona na kupata mapato yake papo hapo baada ya abiria kukata tiketi,”ameeleza Kanali Maiga.

Naye Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Paul Nyello alisema kuwa Serikali imeelekeza kutumika kwa tiketi za kielektroni kwahiyo kila msafirishaji anatakiwa kufuata maelekezo hayo “sisi kama LATRA tunajitahidi kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa matumizi ya mfumo huu lakini endapo itatokea ukiukwaji wa Sheria, hatutosita kuwachukulia hatua,”alisema Bw. Nyello

Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabari Mkoa wa Kilimanjaro SSP Pili Misungwi amewataka abiria kuhakikisha kuwa taarifa zao muhimu zinakuwepo kwenyemfumo waTiketi Mtandao ikiwa ni pamoja na jina, sehemu anapotoka, anapokwenda, muda wa basi kuondoka, kiti alichochagua, nauli iliyokatwa na kadhalika na amewasihi kukagua taarifa hizo ili kujiridhisha kabla ya kuanza safari na pindi wanapobaini kuwa taarifa zilizopo sio sahihi watoe taarifa LATRA au Jeshi la Polisi ili kupata msaada wa haraka.

Vilevile amewataka wasafirishaji kutoa tiketi mtandao kwa abiria, “ninawasihi watoa huduma kufuata agizo la Serikali la kutumia tiketi mtandao ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza maana sisi Jeshi la Polisi tunasimamia Sheria na suala la tiketi mtandao lipo kisheria hivyo kwa msafirishaji atakayekiuka agizo hili atakuwa anakiuka Sheria na hivyo tutamchukulia hatua kulingana na Sheria,” alisisitiza

Bw. Innocent Kimbisa ambaye ni abiria alisema, “naufurahia sana mfumo wa tiketi mtandao kwasababu kwa sasa sisumbuliwi na yeyote, ninachokifanya ni kuingia kwenye mfumo kupitia simu yangu, ninachagua basi ninalolitaka kutokanan na safari yangu, ninalipia na ninaenda moja kwa moja kwenye basi naonesha ujumbe amba ndio tiketi yangu kasha nakaa kwenye kiti nilichochagua bila changamoto yoyote na tena siku hizi hakuna kugombania kiti kama ilivyokuwa zamani,”alisema.

Naye dereva wa basi Bw. alisema kwa mfumo wa tiketi mtandao, kwasasa abiria wana uhakika na safari zao na nauli wanazolipia kwakuwa ndani mfumo zimewekwa nauli elekezi  zinazotolewa na kuidhinishwa na LATRA.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Kodi TRA Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Odupoi Papaa alisema kuwa mfumo wa tiketi mtandao unasaidia Serikali kupata mapato yake ambayo yanaenda kutekeleza masuala mengine ya maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya barabara kwahiyo mwananchi anauhakika kuwa kiwango kilichokatwa kimeifikia Serikali moja kwa moja tofauti na hapo awali.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo