Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KIHENZILE AIAGIZA LATRA KURATIBU USHIRIKISHWAJI NA UANDIKISHAJI WA SACCOS KWA VIKUNDI VYA BODABODA NA BAJAJI
Imewekwa: 15 Feb, 2024
KIHENZILE AIAGIZA LATRA KURATIBU USHIRIKISHWAJI NA UANDIKISHAJI WA SACCOS KWA VIKUNDI VYA BODABODA NA BAJAJI

Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri Uchukuzi ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuratibu ushirikishwaji na uandikishaji wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa madereva wa magurudumu mawili (Bodaboda) na magurudumu matatu (bajaji) nchini kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa usafiri ardhini na kuondoa mivutano baina yao na wasafirishaji wa daladala na mabasi ya abiria.

Mhe. Kihenzile ametoa agizo hilo akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini Mhe.Michael Mwita Kembaki Februari 14, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni Jijini Dodoma.

Vilevile ameitaka LATRA kuwaunganisha madereva katika vikundi vya SACCOS ili kuongeza Udhibiti katika sekta ya Usafiri Ardhini.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuiagiza LATRA kuongeza Udhibiti wa vyombo hivi kwa kuhakikisha jitihada za kuwaunganisha madereva wa bodaboda na bajaji kupitia SACCOS kwa lengo la kuongeza Udhibiti wao pia niwaombe viongozi mbalimbali wa Serikali nchini kuungana na LATRA kuhakikisha bajaji zinatoa huduma kwa mujibu wa Sheria ili kuepusha madhara ya kiuchumi na kijamii”, amesema Mhe. Kihenzile.

Aidha, amewataka madereva bodaboda na bajaji kufuata Kanuni na Sheria kwa kutoingilia huduma za daladala au mabasi ya masafa marefu na kuegesha katika vituo vyao walivyopangiwa huku wakisubiri abiria.

“Kanuni ya 15(h) ya Kanuni za magari ya kukodi inakataza vyombo vinavyodhibitiwa, Kuingilia huduma za daladala au mabasi ya masafa marefu, vilevile LATRA imekua ikikabiliana na changamoto hii ya magari ya kukodi kuegesha katika maeneo ambayo si yao kwa kutoa elimu na kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha tabia hii inakoma”, amesisitiza Mh. Kihenzile.

Kwa upande wake Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabrara LATRA ameeleza kuwa, LATRA imeshaanza majaribio ya SACCOS kwa kuanza na Mkoa wa Kilimanjaro na tayari mafunzo yamefanyika mkoani Arusha na inatarajia kuanza mafunzo Mkoani Dodoma.

“Sisi kama Mamlaka tumepokea maagizo kutoka Bungeni na tayari tumeanza majaribio ya SACCOS mkoani Kilimanjaro na tumefanikiwa kufanya mafunzo mkoani Arusha. Tunatarajia muda wowote SACCOS kuanza Mkoani hapo na Februari hii Mamlaka inatarajia kuanza mafunzo Jijini Dodoma, matarajio ni kufanikisha zoezi hili nchi nzima hadi kufikia Mwisho wa mwaka wa fedha 2024”, ameeleza Bw. Kahatano.

Vilevile, kupitia SACCOS LATRA imekubaliana na vikundi vya bodaboda na bajaji kuwapatia kazi ya kukata leseni kwa niaba ya Mamlaka na kuwapatia kamisheni kwa ajili ya kazi hiyo ili kuimarisha vyama hivyo na kupata mtaji wa kutosha kuweza kujikimu kiuchumi.

“Kufuatia uboreshaji wa huduma zitolewazo na bodaboda na bajaji sisi kama Mamlaka tumekubaliana zifanye kazi chini ya kivuli cha SACCOS na kupitia huu utaratibu tumekubaliana nao kuwapatia kazi ya kukata leseni kwa niaba ya Mamlaka na kwa kufanya hivyo, watapatiwa kamisheni kulingana na mapato watakayo yakusanya ili kuimarisha vyama vyao na kupata mtaji wa kutosha kujiendeleza shughuli zao za kiuchumi, kupitia hiki tunawajengea uwezo wa kujisimamia wao wenyewe”, amesema Bw. Kahatano.

Pia Bw. Kahatano ametoa wito kwa madereva bodaboda na bajaji na vyama vya waendesha vyombo hivyo nchini kufikiria muelekeo wa Mamlaka na wajiandae kupokea mabadiliko ya kuimarisha uchumi wao na kuboresha uhusiano wao.

“Nitoe wito kwa vijana na vyama vya madereva bodaboda na bajaji nchini kufikiria muelekeo ambao Mamlaka umekuja nao na waanze kujipanga kupokea mabadiliko ambayo yana lengo la kuwawezesha wao kiuchumi na kuboresha uhusiano kati ya vikundi vyao na Mamlaka za Serikali”, amefafanua Bw. Kahatano.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo