Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa Taasisi za Wizara ya Uchukuzi zilizofanya vizuri kiutendaji kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Tuzo hiyo imetolewa na Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi na kupokelewa na Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA katika kilele cha Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Tathmini ya Utendaji kazi wa Sekta ya Uchukuzi, Oktoba 25, 2024 Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Bw. Salum Pazzy ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, ambae amesema tuzo hiyo ni muhimu kwa Mamlaka kwa kuwa inatoa mrejesho wa kazi zinazotekelezwa na inaonesha kuwa LATRA imetoa mchango mkubwa katika kuboresha utendaji wa sekta ya uchukuzi nchini.
“Hii inatokana na majukumu mbalimbali tuliyotekeleza kwa weledi na ufanisi ikiwemo kuendelea kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA inayorahisisha utendaji kasi, mfano kwa sasa msafirishaji halazimiki kufika ofisini kufuata leseni ya usafirishaji bali anachapa leseni yake mwenyewe popote alipo na hii imesaidia Mamlaka kupunguza matumizi ya karatasi lakini pia imemsaidia msafirishaji kuokoa gharama na muda,” ameeleza
Vilevile amesema, Mamlaka imeongeza utoaji wa idadi ya leseni za usafirishaji, imeendelea kuandaa na kurusha vipindi vya elimu kwa umma na kusambaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari na maeneo mengine ya kiutendaji jambo ambalo limechangia Mamlaka kuendelea kuwa kinara.
“Tuzo hii tumeipokea kwa furaha na kwetu ni deni, kikubwa tunawaahidi viongozi na wadau wetu kuwa tutaendelea kuchapa kazi na kuongeza ubunifu, pia wategemee utendaji mzuri zaidi ambao utatufanya tuendelee kushika namba moja,” amesema.
Huu ni muendelezo wa ushindi kwa Mamlaka ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 LATRA ilikuwa nafasi ya kwanza kama ilivyo kwa mwaka huu wa fedha na ushindi huo umechagizwa na jitihada za dhati na makusudi zinazotekelezwa na Bodi ya Wakurugenzi LATRA, Menejimenti pamoja na watumishi wote wa Mamlaka hiyo.