Bw. Abdallah Mhagama, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amesema kuwa LATRA itaendelea kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kurahishisha shughuli za kiudhibiti ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi .
Bw. Mhagama amebainisha hayo katika ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Lojistiki na Uchukuzi, Oktoba 18, 2024 uliondaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano Mlimani City Dar es Salaam.
“Mpaka sasa tumefanya mapinduzi makubwa ya Usafiri Ardhini nchini kwenye mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) unaomuwezesha mtoa huduma kama wamiliki wa mabasi na wamiliki wa malori kuomba leseni, kuhuisha leseni, na kufanya malipo kimtandao. Pia, tumefanya maboresho makubwa sana ambapo kwa sasa msafirishaji halazimiki kufika ofisini kuchukua leseni bali anachapa leseni yake mwenyewe popote alipo na haya ni mapinduzi makubwa sana,” ameeleza.
Vilevile Bw. Mhagama amebainisha mifumo mbali mbali inayotumiwa na LATRA ikiwemo Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwenye simu janja na kompyuta kupitia anwani ya www.pis.latra.go.tz pamoja na Mfumo wa Tiketi Mtandao unaomuwezesha abiria kufanya wekesho, kulipia na baadae kupata tiketi kwa njia ya kielektroni.
Kwa Upande wake Dkt. Prosper Mgaya, Mkuu wa Chuo cha NIT ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha sekta ya Uchukuzi na kuhakikisha miundombinu ya usafiri nchini inakuwa bora kama vile usafiri wa reli ambao ulikuwa kama ndoto na sasa imekuwa kweli.
Naye Bw. Andrew Magombana, Mkurugenzi Msaidizi Sekta ya Barabara, Wizara ya Uchukuzi ameeleza kuwa, kwa sasa serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, inafanya mapitio ya Sera ya Uchukuzi, pia wamejifunza kutoka kwa wadau mbalimbali ambao ni watekelezaji wa masuala ya uchukuzi na amesisitiza Wizara itatumia mafanikio ya mkutano huo, mapendekezo pamoja na maoni ya Sera ili kuja na Sera mpya yenye manufaa kwa nchi na sekta ya uchukuzi kwa jumla.
Bw. Patel Ngereza ni Afisa Leseni na Usajili Mwandamizi LATRA na amebainisha mifumo mingine inayotumika ambayo ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo Tumizi wa LATRA App unaopatikana kwa kupakua kwenye simu janja, unaomuwezesha msafirishaji kupata taarifa ya leseni yake na mwananchi kuona nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini (daladala) zilizoidhinishwa na Serikali kupitia LATRA.
Vilevile, amesema LATRA inatumia Mfumo wa e-mrejesho unaomuwezesha, mwananchi kuwasilisha maoni, malalamiko, mapendekezo na pongezi bila ulazima wa kufika ofisini na amewasihi wananchi kutumia mfumo huo ili kuiwezesha Mamlaka kupata mrejesho wa huduma zake na hivyo kufanya maboresho sawasawa na maoni yaliyowasilishwa.