Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA KUONGEZA KASI YA USAJILI WA MADEREVA
Imewekwa: 18 Feb, 2023
LATRA KUONGEZA KASI YA USAJILI WA MADEREVA

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imepanga kuongeza kasi zaidi ya usajili wa madereva ili kupunguza vifo na hasara zitokanazo na ajali za barabarani.

Makakati huo umeelezwa na Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara-LATRA  baada ya kikao cha kupokea taarifa ya uchunguzi wa  ajali za magari zilizotokea Wilayani Kongwa, Mkoani Dodoma na Wilayani Korogwe, Mkoani Tanga kilichofanyika katika ofisi za LATRA mkoa wa Dar es Salaam Februari 16, 2023.

“Tumeweza kupata baadhi ya sababu zilizosababisha ajali lakini pia tumepata mapendekezo ikiwemo kuongeza kasi katika usajili wa madereva hasa kwa mabasi makubwa na mabasi madogo ya kukodi na sisi kama Mamlaka tumekubaliana mpaka kufikia tarehe 28 Februari 2023 madereva wa mabasi madogo ya kukodi wote wawe wameshasajiliwa,” amesema Bw. Kahatano.

Kwa upande wake msimamizi wa uchunguzi wa ajali hizo Bw. Jonathan Mmari amesema ajali zote mbili zilikuwa na sababu zinazoweza kuzuilika hivyo zimetokea kwa uzembe katika safari hizo.

“Sababu za ajali zilikuwa zinazuilika ikiwemo kulipita gari iliyopo mbele mahali ambapo haijaruhusiwa, madereva kutokupata muda mzuri wa kupumzika baada ya safari, mwendo kasi uliopitiliza, abiria kutofunga mkanda wakati wa safari na kuzidisha uzito kwenye gari, hivyo mapendekezo yetu ni magari ya mizigo yafungwe vidhibiti mwendo (VTS), lakini pia madereva wote wapatate mafunzo na wasajiliwe LATRA,” amesema Bw. Mmari.

Kwa upande wake Afisa Viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mha. Prosper Godfrey, ameelezea jukumu la TBS katika kuzuia ajali za barabarani, “Sisi kama TBS tuna kazi ya kuangalia viwango vya magari kama yanafaa kutumika barabarani, tuna kazi ya kuthibitisha magari ambayo yanafanyiwa maboresho kama vile kuongezwa urefu na uzito na kuyapa kibali cha kuendelea kusafirisha, kwa ajali iliyotokea Kongwa lile lori liliongezewa uzito kutoka tani 4 hadi 10 ambapo haikuwa sahihi na wala haikuthibitishwa na TBS.”

Akiongelea Mitaala ya kujifunzia madereva, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Ramadhani Ng’anzi amesema mitaala ya shule za madereva iangaliwe na kufanyiwa maboresho ili kuweza kupata madereva ambao wana weledi.

“Mitaala ya vyuo vya udereva iangaliwe vizuri ili kuweza kutoa mafunzo ambayo yatawafanya madereva kufuata Sheria na Kanuni katika kazi zao hivyo inaweza kupunguza ajali za barabarani, tunaamini chuo kikiwa bora kitatoa madereva bora pia,” amesema SACP Ng’anzi.

Usalama wa Barabarani na safari sio jukumu la Mamlaka za Serikali peke yake bali ni jukumu la kila mmoja, ni wajibu wa dereva kuhakikisha kuwa anaendesha chombo kilicho salama kwa matumizi na kwa mwendo ulio salama, ni jukumu la abiria kumkumbusha dereva wanapoona mwendo  ni hatarishi, jali maisha yako na ya mwenzako

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo