Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA KUONGEZA WIGO WA UDHIBITI
Imewekwa: 27 Feb, 2024
LATRA KUONGEZA WIGO WA UDHIBITI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeaswa kuongeza wigo wa udhibiti mwenendo wa magari mbali na mabasi ya masafa marefu ili kudhibiti mwenendo usiofaa wa madereva hali itakayoweza kupunguza ajali za barabarani.

Wito huu umetolewa na Mhe. Augustine Holle (Mb), Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) aliyemuwakilisha Mhe. Deus Sangu (Mb) Mwenyekiti wa Kamati, baada ya ziara iliyofanyika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Adhini (LATRA) na kukagua shughuli za udhibiti zinazofanywa na Mamlaka ikiwemo ufuatiliaji wa mwenendo wa magari yawapo safarini na uthibitishaji wa madereva, Februari 26, 2024.

Akizungumza baada ya ziara hiyo Mhe. Holle amesema kuwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na LATRA katika kudhibiti ajali, ni wakati wa LATRA kuanza kutumia mifumo yao kudhibiti na magari mengine ili kudhibiti ajali na mwenendo usiofaa wa madereva.

“Tumepita na kuangalia namna mnavyodhibiti ajali kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kizuri zaidi tumeona kuwa mfumo huu haufuatilii mwendokasi pekee, tumeona kuwa unaweza hata kuonesha endapo gari litasimama mahali kwa muda mrefu bila sababu ya msingi, nishauri LATRA mfike hadi kwenye magari mengine tofauti na mabasi ya masafa marefu kama vile magari ya serikali na binafsi ili kupunguza kabisa ajali,” amesema Mhe. Holle.

Aidha, Mhe. Holle ameipongeza Mamlaka kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanya ambayo kwa kiasi kikubwa umewezesha kuwepo kwa uwiano mzuri baina ya wasafirishaji na abiria huku akisisitiza umuhimu wa Mamlaka kubadilika kulingana na eneo husika la kiudhibiti.

Kwa upande wake Prof. Ahmed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA amewashukuru Wajumbe wa Kamati kwa ziara na maoni yao huku akielezea utayari wa Mamlaka kuelekea kufanikisha udhibiti wa mwenendo wa magari kwa magari mengine tofauti na mabasi ya masafa marefu.

“Suala la kudhibiti mwenendo wa magari mengine tofauti na mabasi ya masafa marefu Mamlaka imeshalifikiria na kwa kuanzia tuu magari yetu yote yameunganishwa na mfumo huu, kilichobaki ni kuuboresha mfumo ili uwe na uwezo wa kupakia taarifa za magari mengi zaidi na hili linaendelea, nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa kufika LATRA, mbali na kujionea shughuli zetu pia mmetupa maoni mazuri ya kuboresha huduma zetu zaidi, tumeyapokea na tutafanyia kazi,” amesema Prof. Ame.

Ili kupunguza ajali za barabarani, Mamlaka ilibuni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), huu ni mfumo wa kielekroni unaotumia Satelaiti ili kutoa taarifa za hali ya uendeshaji wa gari husika, taarifa zinazotolewa na mfumo huu ni pamoja na mwendokasi wa gari, kubadili njia (ruti), hali ya ajali na nyingine nyingi.

Kutokana na mfumo huu Mamlaka imefanikiwa kupunguza zaidi ya robo tatu ya ajali ambazo zilikuwa zikitokea nchini pamoja na madhara ambayo yalikuwa yakisababishwa na ajali, mpaka sasa zaidi ya mabasi 7,000 yameunganishwa na Mfumo huu, huku madereva wakipatiwa kitufe cha utambuzi wa dereva (I – Button) ili kuwa na taarifa za dereva anayeendesha gari kwa wakati husika.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo