Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA WATAKIWA KUFUATA SHERIA, KUTOBUGHUDHI ABIRIA
Imewekwa: 23 Nov, 2022
MADEREVA WATAKIWA KUFUATA SHERIA, KUTOBUGHUDHI ABIRIA

Na Mambwana Jumbe

Viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wamewataka madereva wa mabasi ya masafa marefu kufuata Sheria ili kuepusha ajali katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara (LATRA) Bw. Johansen Kahatano na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Ramadhani Ng’anzi Novemba 23, 2022 walipokutana katika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam na kujadili namna bora ya kudhibiti mwendokasi wa mabasi ya masafa marefu kuelekea msimu wa mwisho mwaka.

Aidha, Bw. Kahatano aliwaasa wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini hasa wasafirishaji, madereva, makondakta na mawakala wanaokata tiketi kuzingatia Sheria na kuitii bila shuruti, “sisi hatutakuwa na muhali na mtu yeyote na atakayekiuka Sheria atakumbana na mkono wa Sheria, kwahiyo nawasihi kuwa kila mdau atimize wajibu wake.”

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi ca Usalama Barabarani SACP Ramadhani Ng’anzi alisema kuwa Jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wale wanaokiuka sheria za usalama barabarani wanachukuliwa hatua bila kuoneana aibu, “Tuna imani kuwa madereva ambao wana leseni na wamepitia katika vyuo vya mafunzo ya udereva watafuata kanuni zinazowaongoza barabarani, sisi kama Jeshi la Polisi hatutosita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika anavunja Sheria ya Usalama Barabarani.”

 “Tunashukuru wenzetu wa LATRA wameanzisha mfumo wa tiketi mtandao ambao umesaidia sana kudhibiti wale wanaozidisha nauli kiholela na hivyo nawasihi wale wanaokata tiketi wazikate kwa njia ya mtandao. Kwa madereva nawasihi wafuate kanuni na alama zinazowaelekeza barabarani vinginevyo wasije wakatulaumu," alisisitiza SACP Ng'anzi.

LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabara wanafanya kazi kwa ukaribu kuhakikisha kwamba kunakuwa na udhibiti katika sekta ya usafiri ardhini na hasa katika kuhakikisha kuwa suala la ajali linapungua nchini

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo