Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA NA KAMATI YA USALAMA KUDHIBITI AJALI
Imewekwa: 06 Dec, 2024
LATRA NA KAMATI YA USALAMA KUDHIBITI AJALI

Bw. Geoffrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema, Mamlaka imeazimia kuimarisha Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) hususan katika matumizi sahihi ya Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i- Button) ili kudhibiti ajali za barabarani katika kipindi cha mwisho wa mwaka 2024.

Bw. Silanda amesema hayo katika kikao kazi cha wajumbe wa Kamati ya Uratibu Usalama wa Usafiri Ardhini Desemba 5, 2024 ukumbi wa mikutano ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es salaam.

“Tumejiwekea maazimio ya kila mmoja wetu kuwa na wajibu wa kutekeleza majukumu yake na wenzetu jeshi la Polisi watafuatilia ukaguzi wa magari yanayoanza safari katika vituo mbalimbali na kwa upande wetu sisi LATRA tutahakikisha kuwa mfumo wa VTS unafanya kazi vizuri na tutaweka msisitizo kwenye matumizi ya i- Button ambapo itatusaidia kumtambua dereva anayeendesha chombo kutokana na muda wa safari uliopangwa,” amesema Bw. Silanda.          

Aidha ameeleza kuwa, Mamlaka imeendelea kutekeleza majukumu ambayo imefanya pamoja na kamati hiyo ikiwa ni kwa kufanya ukaguzi endelevu kwa vyombo vya moto kibiashara katika maeneo ya kimkakati, “tumekuwa tukifanya ukaguzi mbalimbali na mwezi Novemba tulifanya katika maeneo ya Mikese Morogoro, Mizani ya Makambako na maeneo mengine katika kila mkoa kuhakikisha hali ya vyombo vya usafiri unakuwa salama,” ameeleza Bw. Silanda

Kwa upande wake Michael Deleli, Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani, ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imejipanga katika kuimarisha usimamizi wa Sheria za usalama barabarani kwa kudhibiti makosa yote ambayo yanaweza kuwa ni viashiria vya ajali za barabrani pamoja na kufanya ukaguzi katika vituo vyote nchini.

“Niwasihi wadau wote wa usimamizi barabarani kuhakikisha muda wote wanasimama kwa pamoja ili idara na kila kitengo kiweze kusimamia Sheria za Barabarani bila kuzivunja kwani utii wa Sheria bila shuruti ni jambo la msingi sana na tukiwa watii hakuna mtu anae weza kuathirika kwa ajali za barabarani” amesema ACP Deleli  

Bw. Ramadhan Msangi, Balozi wa Usalama barabarani ameeleza kuwa, wamekuja na mpango mkakati wa kampeni ya abiria paza sauti ambao utamsaidia abiria kutokalia kimya yale makosa yote ya kisheria yanayopelekea ajali za barabarani.

Naye Bw. Abdallah Mohamed Kiongozi, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) amewasihi madereva kuzingatia Sheria za barabarani kwani wameaminiwa kutunza mali ya wamiliki pamoja na kulinda usalama wa raia na mali zao na hasa kutembea mwendo ambao unakubalika kisheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya LATRA Sura ya 413 kifungu cha 5 imeipa Mamlaka jukumu la kuratibu shughuli za Usalama barabarani na LATRA itakutana tena na Kamati ya Uratibu Usalama wa Usafiri Ardhini mwezi Januari 2025 ili kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio waliyokubaliana na pale ambapo kutabainika changamoto kutafanyika maamuzi ya kuimarisha usalama katika siku zijazo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo