
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ikiongozwa na Prof. Ahmed Mohamed Ame imefanya kikao cha pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA) inayoongozwa na Bw. Mkadam Khamis Mkadam, Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwa lengo la kuboresha ushirikiano pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuendesha shughuli za kiudhibiti kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Kituo cha Ukaguzi wa Vyombo vya Moto, kwa Silva (Dole- Zanzibar) Februari 27, 2025, Prof. Ame amesema kuwa LATRA na ZARTSA ni Mamlaka zinazofanya kazi zinazoshabihiana na hivyo ili kuboresha shughuli za uendeshaji na usimamizi wa huduma za usafiri ardhini, ni muhimu kwa taasisi hizo kuwa na ushirikiano mzuri na maono yanayoendana.
“Lengo kuu la Bodi ya LATRA kuja hapa katika kikao hiki cha mashirikiano ni kuendeleza ushirikiano ambao tulishauanzisha na pia kujifunza masuala kama vile Sheria iliyoanzisha ZARTSA na Sheria nyingine za Kisekta, kufahamu utaratibu wa utoaji wa leseni za vyombo vya moto mnavyovidhibiti pamoja na masharti yake pamoja na kufahamu utaratibu wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto,” amefafanua Prof. Ame.
Naye Bw. Mkadam, Mwenyekiti wa Bodi ya ZARTSA ameeleza kuwa,kikao hicho ni chenye tija kwa taasisi zote mbili ambapo itaandaliwa hati ya maelewano (Memorandum of Understanding) itakayoongeza ushirikiano mzuri na itakayoondoa changamoto kwa wadau wa usafirishaji wa pande zote mbili yaani Tanzania Bara na Zanzibar na hatimaye kunufaika na huduma bora za usafiri ardhini.
Kwa upande wake, Bw. Haji Ali Zubeir, Mkurugenzi Mkuu wa ZARTSA amesema kuwa, LATRA na ZARTSA zitaendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa madereva wa vyombo vya moto vinavyodhibitiwa ili kuongeza uelewa wa matumizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu za usalama barabarani pamoja na kutii Sheria bila shuruti,
Naye, CPA Habibu Juma Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA ameeleza kuwa LATRA inatumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayorahisisha utendaji kazi, utoaji huduma kwa wananchi pamoja na udhibiti kwa jumla.
“Sisi tumetengeneza Mfumo wa Tiketi za Kielektroni ambapo kwa sasa tiketi za mabasi yote ya masafa marefu zinapatikana kwa njia ya mtandao. Tumeruhusu watoa huduma kutengeneza mifumo yao na sisi tunaisajili na imeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa hiyo kodi ya Srikali haipotei. Mfumo pia unatoa orodha ya abiria waliosafiri na taarifa zao muhimu na wakati wowote tukihitaji tunaingia kwenye mfumo. Kwa bahati nzuri tumeingia makubaliano na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ambapo wakati wowote ikitokea dharura ni rahisi kwao kuingia kwenye mfumo na kufahamu nani alikuwepo safarini na kutoa stahiki kwa mujibu wa taratibu zilizopo”, amefafanua CPA Suluo
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA ni taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA) ipo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na taasisi zote mbili zimedhamiria kuendeleza ushirikiano ili kuleta mapinduzi chanya kwa sekta zinazodhibitiwa na hatimaye kila mdau wa usafiri wa ardhini kwa pande zote mbili aweze kunufaika kwa huduma bora zinazotolewa na taasisi hizi kwa Tanzania Bara na Zanzibar.