
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeanza kukagua utekelezaji wa Sheria na Kanuni za udhibiti wa wahudumu kwa mabasi yote ya masafa marefu na kuanzia tarehe 02 Juni, 2025 adhabu zitaendelea kutolewa kwa wanaokiuka Sheria hizo.
Hayo yamebainishwa na Bw, Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA kwenye taarifa iliyotolewa jijini Dodoma Mei 17, 2025.
Katika taarifa hiyo Bw. Pazzy amesema Mamlaka inawakumbusha wamiliki wa vyombo hivyo kutekeleza matakwa ya kanuni ya 22(g) ya Kanuni za Magari ya Abiria za Utoaji wa Leseni za Usafirishaji Tangazo la Serikali Na. 76 la Mwaka 2020 inayomtaka mtoa huduma kuhakikisha mhudumu anayemwajiri amesajiliwa na LATRA.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa wahudumu nao wanatakiwa kutii kanuni ya 20(1)(d) ya Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili Wahudumu wa Magari ya Biashara za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Tangazo la Serikali Na. 81 la Mwaka 2020 zinazomtaka mhudumu wa magari ya kibiashara kuwa na kadi ya usajili iliyotolewa na Mamlaka.
“Tunawakumbusha wahudumu wote kuwasilisha maombi ya kusajiliwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) kwa anwani ya rrims.latra.go.tz au kufika ofisi za LATRA wakiwa na nakala ya Cheti cha Mafunzo na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kusajiliwa na kupatiwa kadi ya usajili” amesisitiza Bw. Pazzy.
Vilevile ameeleza kuwa, katika kutekeleza takwa la Kisheria na Kanuni zake, mwezi Julai 2023, LATRA ilizindua mafunzo ya wahudumu wa mabasi na tarehe 14 Agosti, 2024 Mamlaka ilitangaza tarehe 31 Disemba, 2024 kuwa mwisho wa watoa huduma nchini kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na LATRA huku ikiendelea kutoa elimu na kuwezesha utekelezaji.
Mamlaka ilitangaza tarehe 31 Disemba, 2024 kuwa ni mwisho wa watoa huduma nchini kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na LATRA huku ikiendelea kutoa elimu na kuwezesha utekelezaji ambapo ilizindua mafunzo ya wahudumu wa mabasi Agosti 14, 2024 yanayotolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na Chuo cha Ufundi Arusha kwa utaratibu wa kuwafikia wahitaji.