Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAASWA KUEPUKA RUSHWA
Imewekwa: 24 Jan, 2025
LATRA YAASWA KUEPUKA RUSHWA

Bw. John Shija, Afisa Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) amewaasa watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Bw Shija amebainisha hayo Januari 24, 2025 alipowasilisha mada ya Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mkakati wa Utekelezaji Awamu ya Nne (NCSAPIV) 2023-2030 katika kikao cha Sita cha Baraza la Wafanyakazi la LATRA kinachofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro Crater uliopo katika Jengo la Ngorongoro Jijini Arusha.

Ameeleza kuwa, suala la uwazi kuhusu utaratibu wa kupata huduma za LATRA ni muhimu kwa kuwa, wadau watakuwa na ufahamu wa jinsi ya kupata huduma hizo na hivyo kupunguza mazingira yanayoweza kuashiria mianya ya rushwa, “kufanikisha hili, matumizi ya mifumo ya TEHAMA yatasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuwa mwananchi hatolazimika kukutana na mtumishi pindi anapoomba hadi anapopata huduma anayoitaka hivyo endeleeni kubuni na kuhamasisha matumizi ya mifumo kwenye huduma zenu”.

Ameongeza kuwa, kila mtumishi anapaswa kuwajibika ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na kufahamu athari za ukiukwaji wa taratibu hizo. Pia, ni muhimu watumishi kupatiwa elimu ya maadili na athari za rushwa mahala pa kazi ili wanapotekeleza majukumu yao, wafahamu madhara ya kujihusisha na vitendo hivyo.

“Ili tuweze kuwa na utekelezaji bora wa Mkakati huu, watumishi tunao wajibu wa kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu, hivyo Baraza la Wafanyakazi linawajibika kuhamasisha watumishi mahala pa kazi kuzingatia Maadili na kuchukia Rushwa ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne (NACSAPIV 2023-2030),” ameeleza.

Pia, Bw. Shija amebainisha madhara ya Rushwa kuwa ni kuchelewesha utoaji wa haki kwa wananchi, kuzorota kwa maendeleo ya nchi, kukithiri kwa maovu, kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa, kupunguza uwajibikaji, na kadhalika.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, rushwa ni adui wa haki, hivyo kila mtumishi anapaswa kuchukia vitendo vya rushwa, ukizingatia huduma za Mamlaka zinamgusa kila mtu nchini na hivyo watumishi wawe waadilifu wanapotekeleza majukumu ya Mamlaka siku zote.

“Mtumishi wa umma lazima uwe wa kuaminika, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kupinga na kupambana na vitendo vya rushwa ili kuongeza uadilifu mahali pa kazi, kuwa na utumishi wa umma ulio bora na wenye tija na hatimaye kuleta maendeleo ya taasisi na nchi kwa jumla,” ameeleza CPA Suluo.

Baraza la Wafanyakazi la LATRA linaendesha vikao vyake mara moja kwa mwaka na linajumuisha Wajumbe wa Menejimenti, Wawakilishi wa Watumishi wa Idara na Vitengo, Maofisa Wafawidhi wa Mikoa yote pamoja na Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania –COTWU (T)- Tawi la LATRA.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo