Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAENDELEA KUBORESHA UDHIBITI WA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI NCHINI
Imewekwa: 06 May, 2024
LATRA YAENDELEA KUBORESHA UDHIBITI WA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI NCHINI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha udhibiti wa huduma za usafiri ardhini nchini ili kuboresha hali ya usafiri na kuchochea maendeleo kwa Taifa.

Hayo yamesemwa na Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi alipowasilisha Bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Akizungumzia udhibiti wa usalama wa vyombo vya moto kibiashara, Prof. Mbarawa amesema kuwa, Mamlaka imeendelea na usimamizi wa Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kupitia Kanuni mpya za Matumizi ya VTS ya mwaka 2024 ambazo zimeanza kutumika rasmi Januari 2024.

“Katika kuboresha usimamizi wa VTS, Serikali imeandaa na kutangaza Kanuni za Matumizi ya VTS ya Mwaka 2024 ambazo zilianza kutumika mwezi Januari, 2024 ili kuimarisha Udhibiti na usalama kwa mabasi ya masafa marefu wakati wote kupitia Mfumo wa VTS,” amesema Prof. Mbarawa.

Akiongezea kuhusu mfumo wa VTS Prof. Mbarawa amesema, LATRA imeendelea kusimamia na kufuatilia mwenendo wa vyombo vinavyodhibitiwa na kusaidia kupunguza ajali zitokanazo na mwendokasi na kuongeza ufanisi wa vyombo hivyo.

“LATRA imeendelea kufuatilia mwenendo wa mabasi na vichwa vya treni kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na hadi kufikia Machi, 2024 mabasi 10, 270 na vichwa 20 vya treni (18- TAZARA na 2 – TRC) vimeunganishwa katika mfumo huo hali iliyosaidia kupunguza ajali kwa asilimia 7.26,” amesema Prof. Mbarawa.

Vilevile ameeleza kuwa, ili kuwadhibiti madereva, LATRA imeendelea kusajili na kuwathibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa kwa ajili ya kuimarisha usalama wa huduma za usafiri ardhini.

“LATRA imeendelea kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu wa vyombo vinavyodhibitiwa ili kuboresha ufanisi na usalama, ambapo hadi Machi 2024,  Jumla ya madereva 7,867 wamesajiliwa, madereva  1,441 wakiwa wamethibitishwa na LATRA na kati yao 1,190 wamesajiliwa kwenye mfumo wa VTS na kupatiwa vitufe vya utambuzi wa madereva (i-Button),” ameeleza Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amesema kuwa, Serikali imeiwezesha LATRA kuboresha Mfumo wa tiketi za kielektroni ili kuwawezesha abiria kukata tiketi kwa njia ya mtandao akiwa mahala popote kwa kuanzisha kanuni zinazosimamia mfumo huo.

“Ili kuboresha usimamizi wa tiketi za kielektroni, Serikali imeandaa na kutangaza Kanuni za matumizi ya Tiketi za Kielektroni za mwaka 2024 zilizoanza kutumika Januari, 2024,” amesema Prof. Mbarawa.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inawasihi watumiaji wa vyombo vya moto kibiashara kuendelea kutii Sheria na Kanuni zilizowekwa na Mamlaka ili kuendelea kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo