Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAENDELEA KUIMARISHA USAFIRI ARDHINI KUPITIA TEHAMA
Imewekwa: 16 May, 2025
LATRA YAENDELEA KUIMARISHA USAFIRI ARDHINI KUPITIA TEHAMA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuimarisha utendaji kazi, utoaji wa huduma bora pamoja na usalama wa sekta ya usafiri ardhini kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa katika shughuli za kiudhibiti.

Akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa Fedha 2025/26, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi amesema hadi kufikia Machi, 2025, Mamlaka imeunganisha mabasi yote ya masafa marefu ambayo ni 11,826 yaliyopewa leseni kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa treni za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)  na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

“Mfumo unaonesha kuwa, wastani wa mabasi 8,969 yanatuma taarifa kila siku, sawa na asilimia 76 ya mabasi yote. Aidha, mabasi 2,857 yaliyobaki ambayo ni asilimia 24 ni mabasi yaliyosimama kutoa huduma kwa sababu mbalimbali zikiwemo ajali na matengenezo,” amesema Mhe. Prof. Mbarawa.

Vilevile amesema, ili kuongeza wigo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi, LATRA imewezesha upatikanaji wa taarifa za mabasi kupitia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa anwani https://pis.latra.go.tz/ uliounganishwa na VTS unaowasaidia abiria na wadau wa usafiri nchini kufahamu taarifa za mabasi yanayoelekea vituo vya mabasi vilivyo karibu yao na kuwawezesha wadau hao kufahamu mwendokasi na mahala lilipo basi husika.

Wakati huohuo Mhe. Prof. Mbarawa (Mb) ameeleza kuwa LATRA inaendelea na mchakato wa kujenga dirisha moja la utoaji wa huduma za tiketi za abiria kwa wasafiri wa mabasi ya masafa marefu na wasafiri wa treni za reli ya kisasa (SGR) na reli ya kati (MGR) na kwa sasa dirisha hilo lipo katika hatua za mwisho za kuanza kufanya kazi.

“Hadi sasa mfumo huu kwa upande wa treni unafanya kazi kwa ukamilifu na kwa upande wa mabasi utakamilika mara tu baada ya kukamilika usajili wa mifumo iliyokidhi vigezo vya kuendelea kutoa huduma ya tiketi mtandao ambapo jumla ya mifumo 14 ya watoa huduma imeunganishwa kwenye Mfumo Mkuu wa Tiketi Mtandao, kazi hii ya kuunganisha mifumo inatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, 2025,” ameeleza Mhe. Prof. Mbarawa.

Amebainisha kuwa, LATRA imeendelea kutekeleza jukumu la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu  wa vyombo vya moto kibiashara kupitia mifumo ya TEHAMA.

“Katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Machi, 2025 jumla ya madereva 7,232 walisajiliwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) na kutahiniwa kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (DTS) ambapo kati ya hao madereva 1,550 walithibitishwa na kupatiwa Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i- Button), na Kwa upande wa usajili wa wahudumu hadi kufikia Machi 2025, LATRA ilisajili wahudumu 560 baada ya kupewa mafunzo ambayo yalitolewa kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),” amefafanua Mhe. Prof. Mbarawa.

Kwa upande wa udhibiti usafiri wa waya, Mhe. Prof. Mbarawa amesema Julai 2024 hadi Machi 2025, LATRA ilishirikiana na wadau wa Sekta ya Umma na  Sekta Binafsi kutambua uwepo wa fursa, utayari na mahitaji ya udhibiti wa huduma hiyo nchini ambapo wadau kutoka ndani na nje ya nchi 16 wameonesha utayari wa kuwekeza katika usafiri kwa njia ya waya.

“Kutokana na fursa hiyo, Wizara ya Uchukuzi inaandaa Kanuni za Udhibiti wa Usafiri wa Waya baada ya kupokea maoni ya wadau mwezi Desemba 2024 pamoja na kufanya maombi ya mabadiliko ya muundo wa LATRA ili kuwe na kitengo mahsusi katika udhibiti wa usafiri huo” ameeleza Mhe. Prof. Mbarawa.

Mamlaka inaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anasisitiza matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo