Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAFANYA KAGUZI 275 USAFIRI WA RELI
Imewekwa: 23 Apr, 2025
LATRA YAFANYA KAGUZI 275 USAFIRI WA RELI

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa, kuanzia Februari, 2021 hadi Machi, 2025 Mamlaka imefanya jumla ya kaguzi 275 katika miundombinu ya reli, ishara na mawasiliano, vitembea reli (vichwa na mabehewa) na uendeshaji ambapo kati ya kaguzi hizo, 143 zilikuwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), na kaguzi 132 zilikuwa kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

CPA Suluo, amesema hayo alipoelezea mafanikio ya LATRA ndani ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Aprili 14, 2025, Chuo cha Taifa cha Utalii, Dar es Salaam.

 Amebainisha kuwa, wataalamu kutoka LATRA wamefanya kaguzi mbalimbali za miundombinu ya Reli pamoja na vitembea reli ikiwa ni pamoja na Treni ya Kisasa (SGR) baada ya kuwasili nchini na kabla ya kuanza kutoa huduma ili kudhirisha usalama wake kisha kutoa ithibati.

Kwa upande wa uanzishwaji wa huduma za Treni za SGR, CPA Suluo amesema katika maandalizi ya kuanza kwa huduma za usafiri wa abiria kwa treni za SGR, Mamlaka ilikuwa na jukumu la kuthibitisha ubora wa vitembeareli kabla ya kuanza kutoa huduma.

“Tuliungana na timu ya wataalamu wa TRC na Wizara ya Uchukuzi kwenda Nje ya Nchi kukagua na kuthibitisha ambapo jumla ya vichwa vya treni 17, Mabehewa ya abiria 56, treni za seti za umeme (EMU) 10 na Mabehewa ya mizigo 264 yamekaguliwa kipindi cha uundwaji katika nchi za Korea, China, Malaysia na Ujerumani. Pia Mamlaka imefanya kaguzi za majaribio kwa mabehewa na vichwa hivyo baada ya kuwasili nchini kabla ya kuanza kutumika kutoa huduma,” amefafanua CPA Suluo.

Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya usafiri ardhini nchini ikiwemo usafiri wa reli ambapo tumeshuhudia uanzishwaji na uendeshwaji wa treni za kisasa (SGR) uliozinduliwa rasmi jijini Dodoma Agosti 1, 2024 na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Usafiri huu umechochea ongezeko la uchumi wa wananchi na Serikali kwa jumla na umekuwa ni usafiri salama na unaoaminika uliochagizwa na kaguzi zinazofanywa na LATRA kwa uweledi na ufanisi hivyo kuongeza tija ya huduma za usafiri huu nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo