Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAJIKITA KUSIMAMIA USAFIRI SALAMA
Imewekwa: 10 Oct, 2023
LATRA YAJIKITA KUSIMAMIA USAFIRI SALAMA

Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Zakaria Saili Mwansasu, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuendelea kusimamia Sheria na Kanuni za usafiri ardhini, kuboresha huduma za usafiri nchini na kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali na maafa yatokanayo na matumizi mabaya ya vyombo vya usafirishaji.  

Ameyasema hayo tarehe 9 Oktoba, 2023 kwa niaba ya Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Buriani, Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli yanayofanyika nchi za Jumuiya ya Mashirika ya Reli ya Kusini mwa Afrika (SARA) ambapo kwa upande wa Tanzania, maadhimisho haya yanafanyika Kitaifa Mkoani Tabora.

Aidha, amesisitiza kufanyika maboresho ya mfumo wa Tiketi Mtandao ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa abiria wa treni ikiwa ni pamoja na kuzuia mianya ya upotevu wa fedha za Serikali katika huduma za reli.

“Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza LATRA kwa hatua wanazochukua na kulielekeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuboresha Mfumo wa Tiketi Mtandao kwa abiria wa treni ili wajikatie tiketi zao wenyewe popote walipo kwa njia ya mtandao” Amesema Mhe. Mwansasu.

Aliongeza kuwa, maelekezo hayo ni muendelezo wa maagizo ya Serikali yaliyotolewa na Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya TRC hivi karibuni.

“Haya pia ni maagizo ya Serikali yaliyosisitizwa na mambo haya yamewezekana kwenye usafiri wa mabasi zaidi ya 8,500 nchini, hatuoni sababu ya kutowezekana kwa TRC. Kwa ujumla, tunaona mabadiliko makubwa katika sekta ya reli yanakuja hapa Nchini. Kwa hili nawapongeza sana LATRA. Endeleeni kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, na kila mmoja atimize wajibu wake ili watanzania wafurahie huduma bora na salama za usafiri wa reli,” aliongeza Mhe. Mwansasu.

Vilevile, Mhe. Mwansasu amewasisitiza wananchi kutembelea maonesho hayo ili waweze kupata elimu inayohusiana na usalama wa reli pamoja na kulinda miundo mbinu ya reli nchini huku wakizingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “usalama unaanza na wewe chukua tahadhari’’ kwa kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha usafiri wa reli unakuwa salama kwa kushirikiana na wananchi.

 “Tuwe walinzi wa miundombinu kwa maendeleo ya nchi yetu na nisisitize katika maeneo yote ambayo alama za usalama wa reli zimeondolewa ziwekwe upya mapema kwa ajili ya kuimarisha usalama wa usafiri wa reli, abiria na mali zao kwa ujumla” alisisitiza Mhe. Mwansasu.

Kwa upande wake Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA amemshukuru Mhe. Mwansasu kwa pongezi alizozitoa na kuahidi kuwa LATRA itaendelea kuboresha udhibiti wa huduma za usafiri ili kuongeza tija na kukuza uchumi.

“Nipende kuwasihi TRC, TAZARA na LATRA kusimamia vizuri usalama wa reli mpaka kufikia asilimia 100, kuwahakishia na kuwaaminisha wananchi na wadau wote kuwa usafiri wa reli ni salama na haraka ndipo tutakapo kuza uchumi wetu,” amesema Prof. Ame.

Naye, CPA Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, amewapongeza madereva bodaboda wa mkoani Tabora, waliofuzu mafunzo ya udereva yaliyowezeshwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na kupatiwa vyeti katika hafla hiyo ambapo ameahidi kutoa ushirikiano kwa madereva hao na kuwasihi vijana wengine wajitokeze kupata mafunzo.

“Sisi LATRA tunafarijika sana na juhudi hizi za madereva wa bodaboda zinazorahisisha udhibiti, tunawasihi kujiunga katika umoja wa vyama vya ushirika kama SACCOS na LATRA itawatambua na tunaahidi kuwapa vitendea kazi ili waweze kujidhibiti wenyewe na kujiongezea kipato,” amesema CPA Suluo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo