
INSP Blandina Kasongwa, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kufungua ofisi mji wa Ifakara ambayo imeongeza tija kwa kutatua changamoto mbalimbali za usafiri na usafirishaji kwa wadau usafiri ardhini.
INSP Kasongwa amesema hayo Februari 06, 2025 Wilayani Kilombero ambapo LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabani, walitoa elimu ya Uthibitishwaji wa madereva na Usajili wa wahudumu kwa madereva na mawakala wa mabasi ya masafa marefu mji mdogo Ifakara Wilayani hapo.
“Kipindi hatuna ofisi za LATRA kwa hapa Ifakara kwa kweli palikuwa na changamoto kubwa sana na wasafirishaji wengi hawakuwa na leseni za LATRA, lakini baada ya kusogezewa huduma karibu, mtu mwenye changamoto na dharura yoyote, LATRA imekuwa ikitatua changamoto izo kwa urahisi na haraka, na kimsingi LATRA kufungua ofisi Ifakara imepunguza ajali wilayani hapa kwa kuwa magari yote lazima yafanyiwe ukaguzi ndipo yapate leseni za LATRA” amesisitiza INSP. Kasongwa.
Naye Bw. Amani Mwakelebela, Afisa Mfawidhi LATRA Ifakara ameeleza kuwa kifungu cha (4)(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini sura ya 413 kinamtaka kila dereva anayeendesha chombo cha moto kibiashara awe amesajiliwa na kuthibitishwa na LATRA, hivyo ni wajibu wa madereva wa vyombo vunavyodhibitiwa na Mamlaka kufanya hivyo ili watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
“Dereva anapaswa kuthibitishwa baada ya kufanya mtihani wa kupimwa uelewa wake kwa kazi anazozifanya na akifaulu atapatiwa cheti na Mamlaka kitakachoongeza wigo wa ajira kwani ataweza kuajiriwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania hususan katika Jumuia za Africa Mashariki. Tunasisitiza madereva mjitokeze kwa wingi ili kunufaika na fursa lukuki zinazopatikana baada ya kutahiniwa na kuthibitishwa na LATRA”, ameeleza Bw. Mwakalebela.
Naye Bw. Ally Haji Dereva wa mabasi ya masafa marefu Ifakara ambaye amesajiliwa na LATRA amesema, “Naishukuru sana Serikali kwa kuiwezesha LATRA kufika Wilaya ya Kilombero mji mdogo wa Ifakara na kutufikishia huduma ambazo mwanzo ilitulazimu kuzifuata mjini Morogoro, lakini sasa zimefika karibu na tunazipata kwa urahisi na tutaendelea kuwakumbusha wenzetu ambao bado hawajathibitishwa ili wafanye hivyo.”
Tangu Kuanzishwa kwa ofisi ya LATRA Wilaya ya Kilombero mji mdogo wa Ifakara Mkoani Morogoro mwezi wa sita mwaka 2024, mwitikio wa ukataji leseni za LATRA umeongezeka na wadau wa usafirishaji wakiwemo wamiliki na madereva wa vyombo vya moto kibiashara wamefanikiwa kutatua changamoto zao kwa wakati.