
Mhe. Jamal Abubakar, Mwenyekiti wa Kamati ya siasa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mchafukoge ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuendelea kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.
Mhe. Jamal amesema hayo kwenye kikao kati ya Kamati ya siasa CCM Kata ya Mchafukoge na LATRA kilichofanyika Februari 3, 2025 ukumbi wa Mikutano ofisi za LATRA Dar es Salaam.
“Nawapongeza sana kwa jitihada mnayofanya kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kwakuwa imeongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yenu kwani mnafanya vizuri katika kusimamia sekta ya usafiri na kuhakikisha huduma zinakuwa bora kwa wananchi,” amesema Mhe. Jamal.
Katika kikao hicho Bw.Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ameielezea mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na LATRA katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo imerahisisha utoaji huduma kwa wasafirishaji na wananchi.
“Miongoni mwa mafanikio tunayojivunia ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ulio rahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wa dereva anapokuwa safarini na kupunguza ajali za barabarani pia Mamlaka imerahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi kupitia Mfumo wa PIS (Mfumo wa Taarifa kwa Abiria) unaomuwezesha abiria kufahamu taarifa za mabasi yanayowasili katika vituo vya mabasi nchini na mwendokasi wa basi,” ameeleza Bw. Pazzy.
Aidha Bw. Pazzy ameitaja mifumo mingine kuwa ni, Mfumo Tumizi wa LATRA App unaomuwezesha mwananchi kufahamu nauli zilizoidhinishwa na LATRA, pamoja na kuhakiki uhai wa leseni, Mfumo wa huduma kwa wateja ambao unatumiwa kuwasiliana na wateja moja kwa moja siku zote kupitia namba bila malipo 0800110019 au 0800110020.
Vilevile amesema LATRA inajivunia utoaji wa huduma za safari za saa 24 zilizoanza kutolewa rasmi tarehe 1 Oktoba, 2023 nakuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Bw. William Masai, Afisa Leseni na Usajili LATRA ameieleza kamati hiyo kuwa, LATRA inafanya kila jitihada kuendelea kuboresha huduma za usafiri wa mjini zinazotolewa na daladala ili kuweza kuwafikia watanzania mbalimbali.
“Kupitia elimu mbalimbali na ukaguzi endelevu tunaendelea kuboresha huduma za usafiri wa daladala na kutatua changamoto mbalimbali za usafiri huu na tumeweza kuweka idadi maalum katika njia mbalimbali ili kurahisisha huduma za usafiri nchini,” amesema Bw. Masai.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 10 akiwemo Mhe. Mariam Lulida, Diwani Kata ya Mchafukoge pamoja na Baadhi ya maafisa kutoka LATRA.