Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imepongezwa kwa kubuni Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuitumia mifumo hiyo katika utendaji kazi wa kila siku jambo linaloongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wadau wake.
Pongezi hizo zimetolewa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) alipotembelea banda la LATRA, viwanja vya Nzuguni - Dodoma kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa – Nane Nane, Agosti 6, 2024.
Dkt. Chang’a amesema, “Nawapongeza kwa kubuni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) pamoja na Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) uliotengenezwa na wataalam wetu wa ndani na umekuwa na manufaa makubwa kwa Serikali, Wasafirishaji na Wananchi kwa jumla.”
Naye Bw. Hamza Johari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ameipongeza LATRA kwa kazi nzuri ya kiudhibiti inayoifanya kwa kuwa suala zima la usalama wa usafiri ardhini umeongezeka na unaridhisha.
“Tumeshuhudia usalama wa usafiri ardhini kwa maana ya usafiri wa barabara na pia kwa usafiri wa reli ambao kwa sasa tumeona usafiri kwa treni ya kisasa ya SGR umeanza kwa kasi katika Taifa letu na hiki ni kielelezo tosha kwamba LATRA inatekeleza majukumu yake kwa kiwango cha hali ya juu,” ameeleza Bw. Johari.
Vilevile Bw. Johari, amesema amefurahishwa na Mfumo wa PIS unaomwezesha mwananchi kuangalia mwendokasi wa basi alilopanda na endapo basi husika lina mwendo hatarishi, anawasiliana na LATRA kwa kuwapigia simu na wao wanashughulikia jambo hilo kwa wakati.
“Tumeshudia uboreshaji wa huduma mbalimbali kimtandao kama vile matumizi ya Mfumo wa Tiketi Mtandao ambapo kwa sasa unaweza kununua tiketi kupitia simu yako janja ya mkononi popote ulipo, kwa wakati wowote na kufanya wekesho (booking) bila kulazimika kwenda kituo cha mabasi kufuata huduma hiyo, haya ni maendeleo makubwa sana,” amesema Bw. Johari,
Wadau mbalimbali waliotembelea banda la LATRA kwenye Maonesho ya Nane Nane - Dodoma wameeleza kuwa kwa sasa mambo huduma za usafiri ardhini zimerahisishwa kama vile kwa kutumia Mfumo wa PIS, wanafuatilia vituo vya mabasi pamoja na kufahamu muda mwafaka wa kuwasili kule wanakoenda na hata kama wana ndugu anayetoka mkoa mwingine, wanatazama kwenye mfumo na kuona muda atakaofika.
Bi. Alicia Sebastian, ni mmoja wa wadau na anaeleza kuwa, kupitia maonesho hayo amejifunza LATRA inavyodhibiti mabasi na vyombo vya usafiri vinavyofanya biashara ardhini pamoja na mifumo ya TEHAMA na jinsi ilivyorahisisha upatikanaji wa taarifa za LATRA na usafiri kwa jumla.
Kwa upande wake, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, LATRA itaendelea kutekeleza jukumu lake la kiudhibiti kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini zilizowekwa na wataendelea kushirikiana na wadau katika kila hatua ili kuwa na usafiri wa ardhini ulio salama na wenye tija kwa wote.
Pia, amewasihi madereva wa vyombo vya moto vinavyodhibitiwa ambao bado hawajasajiliwa na kuthibitishwa na LATRA wafanye hivyo na amewataka madereva wote waliothibitishwa kutumia kitufe cha utambuzi wa dereva (i-button) wakati wote wa safari na kufanya vinginevyo ni kinyume cha Sheria na Kanuni zilizopo na hivyo watachukuliwa hatua stahiki pindi watakapokutwa bila kitufe hicho.
Mamlaka inashiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa – Nane Nane yanayofanyika viwanja vya Nzuguni - Dodoma kuanzia Agosti 01-08, 2024. LATRA ni mdau mkubwa wa sekta ya Kilimo kwa kuwa ndiyo Taasisi ya Umma inayotoa leseni za usafirishaji inayowezesha usafirishaji wa pembejeo za kilimo na mazao kutoka shambani hadi kwa mlaji.