Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA FIMBO NYEUPE DUNIANI
Imewekwa: 22 Oct, 2022
LATRA YASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA FIMBO NYEUPE DUNIANI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini imeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe Duniani yaliyofanyika Kitaifa mjini Babati mkoani Manyara kuanzia tarehe 19 hadi 21 Oktoba, 2022 yenye kaulimbiu ‘Ujumuishwaji wa Watu wasioona katika Ajira, Michezo na TEHAMA kwa Maendeleo Endelevu’.

Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwa niaba ya Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, Mhe. Katambi alisema, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maagizo yake amefanya mambo mengi yanayoitekeleza kaulimbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na utoaji wa ajira, ujumuishwaji katika maswala ya TEHAMA, uboreshaji wa elimu, uweshaji kupitia mikopo na upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.

“Serikali ya awamu ya sita imeendelea kujipambanua kwa kuitekeleza Sheria namba 9 ya mwaka 2010 na Sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, ambapo mwaka huu 2022, kati ya ajira 9,800 zilizotolewa Serikalini, viliwekwa viwango vya chini maalum kwa watu wenye ulemavu, hivyo kuwezesha watu wenye ulemavu 261 kuajiriwa, kati yao 61 ni wasioona,” alisema.

Aliongeza kuwa, mwaka huu, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa agizo la ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala ya TEHAMA na Serikali imeendelea kuwatambua, kuwasikiliza na Kutatua changamoto zao katika nyanja mbalimbali.

“Serikaili inatambua umuhimu na inathamini watu wenye ulemavu, kwa sababu tunajua, hujafa hujaumbika. Serikali imepunguza kodi kwa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu. Kulikuwa na vyuo 7 ambavyo vilikuwa havifanyi kazi, Serikali imevifufua vyuo hivyo ikiwemo chuo cha Ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu cha Masiwani kilichopo mkoani Tanga,” alifafanua.

Aidha, Mhe. Katambi alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010, taasisi yoyote inayoajiri watu zaidi ya 20, asilimia 3 wanatakiwa waajiriwe watu wenye ulemavu.

“Tutakagua hadi kwenye viwanda, kama huna watu wenye ulemavu basi ujue unavunja Sheria. Nawaagiza maafisa kazi, ukaguzi ufanyike maeneo yote yanayotoa ajira muhakikishe Sheria hii inazingatiwa. Pia napenda kuwajulisha kuwa Mheshimiwa Rais ametoa fedha kuwezesha utengenezaji wa mafuta ya ngozi kwa ajili ya watu wenye ulemavu unaofanyika hospitali ya KCMC na hatuna upungufu.”

Pia Mhe. Katambi ametoa wito kwa Mamlaka mbalimbali kuwezesha fimbo nyeupe iwe sehemu ya utaratibu wa alama za barabarani na Sheria itoe adhabu kali kwa wataovunja utaratibu huo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Manyara amewashukuru wafadhili waliowezesha maadhimisho hayo ambao ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, ambapo maadhimisho hayo yamewezesha wadau kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo changamoto wanazokabiliana nazo watu wasioona na namna ya kuzitatua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu J. Suluo alisema kuwa Mamlaka hiyo inatambua na kujali jamii ya watu wenye mahitaji maalum, pia kwa mujibu wa Sheria ya LATRA, kifungu cha 6 (e), Mamlaka ina wajibu wa Kuimarisha Ustawi wa Jamii ya Kitanzania kwa Kuboresha upatikanaji wa huduma za Usafiri Ardhini kwa watumiaji wote ikiwemo wenye kipato cha chini, watu wa vijijini na watu wenye mahitaji maalum. Hivyo, LATRA inaposhirikiana na wadau wa fimbo nyeupe, inatekeleza jukumu la Kisheria.

“Tunaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili mtu asiyeona apate haki zake na ajue wajibu wake anapotumia huduma za usafiri ardhini.” Alisema

Alifafanua kuwa, mwaka 2019, Mamlaka ilichapisha nakala 130 za toleo la nukta nundu (braille) la Kanuni za Leseni za Usafirishaji kwa Magari ya Abiria na kuzigawa kwa watu wasioona kupitia Chama cha Wasioona Nchini ikiwa ni sehemu ya kuwaelimisha watu wenye ulemavu ili nao washiriki katika maboresho ya kanuni za leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria wakati wa kuandaa kanuni hizo.

“Kwa kuwa LATRA iliwashirikisha walemavu, Kanuni za Leseni za Usafirishaji kwa Magari ya Abiria, zilizochapishwa mwaka 2020, zinahusisha haki za walemavu, kwa mfano kanuni hizo zinamruhusu mlemavu kusafiri na kiti chake maalum bila kulipia gharama za ziada.” Alisisitiza

Aidha, CPA Suluo alisema, LATRA imekua ikishirikiana na Taasisi ya Wasioona (TLB) katika kutoa elimu mbalimbali ikiwemo elimu ya ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ambapo kwa sasa, Mamlaka inachapisha nakala 50 katika maandishi ya nukta nundu za Muongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu uliotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora unaoainisha haki na wajibu wa watumishi wa Umma wenye ulemavu na haki na wajibu wa waajiri ili kujenga mazingira wezeshi..

“Jana katika Semina yetu hapa mmefundishwa na mtu asiyeona wa hapahapa Manyara, jinsi ya kukata tiketi kwa njia ya mtandao na tuligawa makabrasha yaliyoandikwa katika mfumo wa nukta nundu,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Bw. Omari Mpondelwa alisema kuwa uimara wa chama hicho unategemea aimara wa wanachama, uimara wa Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kutatua changamoto za watu wasioona ambazo ni nyingi.

“Zipo changamoto za unyanyapaa na zingine za watu kutokujua kwa kufanya huruma iliyopindukia. Nawahimiza wanachama kuendeleza umoja na mshikamano utakaotoa taswira nzuri kwa wadau mbalimbali kushirikiana na wasioona kuleta maendeleo,” alisema.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo