Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YASOGEZA HUDUMA ZA USAFIRI KARIBU NA WANANCHI
Imewekwa: 14 Apr, 2025
LATRA YASOGEZA HUDUMA ZA USAFIRI KARIBU NA WANANCHI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kusogeza huduma za usafiri ardhini karibu na wananchi kwa lengo la kuboresha sekta ya usafiri nchini.

Amebainisha hayo CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, alipowasilisha mafanikio ya LATRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Aprili 14, 2025, Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dar es Salaam.

 “Tumefungua ofisi kumi (10) maeneo ya kimkakati kwenye baadhi ya Halmashari za Miji na Wilaya nchini. Maeneo hayo ni Kituo cha Mabasi Magufuli - Mbezi, Tegeta, na Mbagala (Dar es Salaam), Makambako (Njombe), Kahama (Shinyanga), Masasi (Mtwara), Ifakara (Morogoro), Korogwe (Tanga), Same (Kilimanjaro), na Nzega (Tabora),” amesema CPA Suluo.

CPA Suluo ameongeza kuwa, Mamlaka inaendelea na juhudi za kusogeza huduma za LATRA karibu na wananchi na taratibu  za kuanzisha Ofisi nyingine tano (5) zinaendelea katika maeneo ya Gongo la Mboto (Dar es Salaam), Mkuranga (Pwani), Chunya (Mbeya), Mufindi (Iringa), na Nyakanazi (Kagera).

Vilevile CPA Suluo ameeleza jinsi ofisi ndogo za Mamlaka zilizvyowafikia wananchi na wadau, “kufikia mwezi Machi 2025, ofisi hizi ndogo zimeonesha mafanikio katika kufikia wananchi walio mbali na miji mikuu ya mikoa, kuboresha udhibiti wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda), kutatua migogoro ya wadau katika maeneo hayo, kufikisha elimu kwa wadau na kusogeza ushirikiano na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo hayo, ikiwemo Serikali za Mitaa (LGAs), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mamlaka zingine zilizopo kwenye maeneo hayo.

Wakati huohuo,  CPA Suluo ameeleza kuwa Mamlaka imeendelea kusogeza huduma za usafiri wa miji na majiji karibu na wananchi katika maeneo yenye changamoto za usafiri kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa.  

 “LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa hapa nchini, na imeanzisha njia mpya 1,007 za daladala Mkoani Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi vilevile katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Arusha imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma,” ameeleza CPA Suluo.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo