Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATANGAZA NAULI MPYA MABASI YAENDAYO HARAKA, TEKSI MTANDAO
Imewekwa: 03 Jan, 2023
LATRA YATANGAZA NAULI MPYA MABASI YAENDAYO HARAKA, TEKSI MTANDAO

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli mpya za teksi mtandao, pikipiki mtandao na mabasi yaendayo haraka (BRT) zitakazotumika nchini siku 14 kuanzia sasa. Nauli hizo zimetangazwa Januari 3, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu Suluo jijini Dodoma.

Akizungumza na Wanahabari, CPA Suluo amesema, tangazo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, ambapo LATRA imepewa jukumu la kupanga nauli za vyombo vinavyotoa huduma za usafiri ardhini kibiashara.

Nauli mpya kwa mabasi yaendayo haraka ni shilingi 750 kutoka shilingi 650 iliyokuwa awali kwa njia kuu na shilingi 500 kutoka shilingi 400 kwa njia mlisho sawa na ongezeko la shilingi 100, abiria watakaounganisha njia kuu na njia mlisho watalipia shilingi 900 na kwa njia ya Kimara hadi Kibaha watalipia shilingi 700.

CPA Suluo amefafanua kuwa, teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi wanne (4) kiwango cha chini kitakuwa shilingi 3,000 na kiwango cha juu kitakuwa shilingi 4,000 kwa safari isiyozidi kilometa moja. Aidha, nauli ya kuanzia safari ni shilingi 500 hadi 1,000, nauli kwa kilomita ni shilingi 800 hadi 1,000, nauli kwa dakika ni shilingi 80 hadi 100. 

Vilevile, teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi sita (6) nauli ni shilingi 4000 hadi 5000 kwa safari isiyozidi kilomita moja. Nauli ya kuanzia safari ni shilingi 800 hadi 1,300, nauli kwa kilometa ni shilingi 1,000 hadi 1,200, nauli kwa dakika ni shilingi 80 hadi 150.   

Kwa upande wa pikipiki mtandano nauli mpya kwa pikipiki zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi wawili (2) ni shilingi 1,000 hadi 1,500, nauli ya kuanzia safari ni shilingi 250 hadi 350, nauli kwa kilomita ni shilingi 300 hadi 400, nauli kwa dakika ni shilingi 50 hadi 70. 

Na kwa pikipiki zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi watatu (3) nauli ni shilingi 2,000 hadi 2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja, nauli ya kuanzia safari ni shilingi 350  hadi 500, nauli kwa kilomita ni shilingi 500 hadi 600, nauli kwa dakika ni shilingi 70 hadi 90. 

Aidha CPA Suluo amesisitiza kuwa, nauli zitakazotumika katika mabasi yaendayo haraka ni zile zilizotangazwa na Mamlaka na kuwa mfumo wa utoaji tiketi utakaokubalika ni wa kielektroni au kadi ambazo zinakubalika na watoa huduma.

“Nipende kuwakumbusha watoa huduma wa haya mabasi yaendayo haraka kuwa, nauli wanazopaswa kutoza ni hizi tulizozitangaza, na tiketi halali ni zile zinazotolewa kwa njia ya kielektroni au zile kadi ambazo za kusafiria zinakubalika” amesema CPA Suluo.

 

 

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo