Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATEKELEZA MIKAKATI KUBORESHA USAFIRI WA RELI NCHINI
Imewekwa: 27 Sep, 2022
LATRA YATEKELEZA MIKAKATI KUBORESHA USAFIRI WA RELI NCHINI

Na. Salum Pazzy

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu J. Suluo amesema kuwa, LATRA imejipanga kuimarisha huduma za udhibiti usafiri ardhini nchini ikiwemo usafiri wa reli ili kufikia azma ya Serikali kuwezesha usafiri bora na salama kote nchini.

Ameyasema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo yanayotolewa kwa wafanyakazi wanaoshughulikia uendeshaji wa treni moja kwa moja yaliyoandaliwa na LATRA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia yanayofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Tabora na Morogoro na kuwafikia wafanyakazi zaidi ya 150 kutoka mikoa yenye usafiri wa reli nchini.

Aliongeza kuwa, LATRA imeongeza mikakati ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wanaoshughulikia uendeshaji wa treni moja kwa moja kwa kuwa Raslimali watu ni raslimali muhimu na ghali zaidi. Watu wanaweza kuongeza au kupunguza ufanisi wa shirika la reli kulinganga na jinsi wanavyotekeleza kazi zao.

“Zaidi ya silimia 90 ya ajali za treni zinasababishwa na makosa ya kibinadamu, hii inatokana na kutozingatia miongozo yetu katika utendaji. Ninawasihi, kila mmoja azingatie mafunzo haya na akayafanyie kazi ipasavyo. Ajali ni kiashiria kikubwa cha mapungufu katika uendeshaji wa treni zetu. Ajali hizi zinaleta hasara kubwa kwa kupoteza maisha ya watu, kuharibu miundombinu ya reli na mali,” alisema

Aidha CPA Suluo alisisitiza kuwa, ajali inapotokea, kila mmoja ajitathmini iwapo alitimiza wajibu wake ipasavyo. Ikitokea watu wamepoteza maisha kwa sababu mmoja wetu hakutimiza wajibu wake, mtu huyo anakuwa ametenda makosa makubwa kwa mujibu wa miongozo ya utendaji kazi na ni dhambi kubwa hata katika Imani yake.

“Reli zetu zinategemewa sana katika usafirishaji ndani na nje ya nchi, ikiwemo nchi ambazo hazifikiwi na bahari. Huduma zetu ni lazima ziwe shindani kwa kuwa wateja wanauwezo wa kutumia huduma mbadala na kuacha huduma zetu zikiendeshwa kwa hasara,” alifafanua

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Reli Mhandisi Hanya Mbawala, alisema kuwa, baada ya mafunzo hayo kukamilika, itatafanyika tathmini ya kujua matokeo na mapokeo ya mafunzo haya yaliyopangwa kufanyika kwa ngazi zote za watendaji wa TRC.

“Wafanyakazi hawa ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo wanaofanya TRC itekeleze kazi zake ipasavyo. Baada ya mafunzo kwa ngazi hii ya watendaji wa moja kwa moja, tutawafanyia mafunzo ngazi ya menejimenti na hatimaye hadi ngazi ya Bodi ya Wakurugenzi, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa wapamoja katika kuboresha huduma za usafiri wa reli nchini ikiwemo reli ya Kisasa inayotarajiwa kuanza kufanya kazi hapo baadaye,” alisema Mhandisi Hanya

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo