Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATOA ELIMU KWA MADEREVA NA WAMILIKI WA PIKIPIKI WILAYA YA SAME-KILIMANJARO
Imewekwa: 08 Feb, 2025
LATRA YATOA ELIMU KWA MADEREVA NA WAMILIKI WA PIKIPIKI WILAYA YA SAME-KILIMANJARO

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imetoa elimu kuhusu kazi na majukumu ya LATRA, ukataji wa leseni za LATRA kwa pikipiki za magurudumu mawili pamoja na Usajili wahudumu na uthibitishwaji wa madereva kwa wadau wa usafirishaji hususan Madereva na Wamiliki wa  Pikipiki za Magurudumu Mawili, katika vituo mbalimbali vya bodaboda wilayani Same - Kilimanjaro Februari 4, 2025.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu Bw. Salum Pazzy Mkuu wa kitengo Uhusiano na Mawasiliano LATRA ameelezea  umuhimu wa kuwa na leseni za LATRA kwa wasafirishaji hao pamoja  na kuunda vyama vya Ushirika (SACCOS) kwa wanachama hao.

“Ukataji wa leseni za LATRA ni takwa la kisheria ndio maana LATRA tumesogeza huduma wilayani hapa, vile vile LATRA imewaletea jambo jema ambapo kwa umoja wenu mkiungana mnaweza kuunda chama cha ushirika (SACCOS) kitakacho wainua kiuchumi kwa kurudisha asilimia ishirini ya mapato mnayokusanya kuleta LATRA serikali imeleta fursa na mnapaswa kuzichangamkia” ameeleza Bw. Pazzy.

Aidha Bw. Frank Sanga kaimu afisa mfawidhi LATRA Wilaya ya Same-Kilimanjaro, ameelezea tija ya LATRA kuwa na ofisi Wilayani hapo ambayo imeleta tija kubwa kwa kuhamasisha madereva na wamiliki wa pikipiki za magurudumu mawili juu ya ukataji leseni za LATRA na kuelezea jinsi ambavyo ofisi ya LATRA Wilaya ya Same inashirikiana na jeshi la polisi wilayani hapo.

“Kwa sasa  madereva na wamiliki wa pikipiki za magurudumu mawili wanajitokeza kwa hiari kuja kukata leseni za LATRA ishara ambayo inaonyesha muamko na mwanga kwetu LATRA lakini pia  tunashirikiana kwa karibu na jeshi la polisi, hawa ni wenzetu na hata ukimkuta bodaboda amekiuka taratibu na kupita  eneo lenu la ukaguzi ukimwomba askari, huwa anamsimamisha na tunampa elimu” amefafanua Bw. Sanga.

Naye  Bw. Amos Alfred katibu wa madereva wa pikipiki za magurudumu mawili kituo cha bodaboda halmashauri ya wilayani Same -  Kilimanjaro  ameipongeza LATRA kwa kufika kwenye kituo hicho  na kutoa elimu hususan kuwa wakala wa utoaji wa leseni za LATRA.

“Kituo kama hiki kinaweza kuwa wakala wa ukataji wa leseni za LATRA ambacho kinaweza kutoa huduma kwa niaba ya LATRA lakini pia kuleta ukaribu wa huduma kwa waendesha pikipiki za magurudumu mawili ambao wapo kwenye  kituo hiki na vituo vingine “ameeleza Bw. Alfred.

Vilevile Bw. Chedieli Mgonja ameishukuru na kuipongeza LATRA kwa kufikisha elimu wilayani same na jinsi ambavyo mwitikio wa madereva wa pikipiki za magurudumu mawili umebadilisha mtazamo wao juu ya LATRA na kupata uelewa wa faida za kukata leseni ya LATRA na kuunda vyama vya Ushirika.

“Tunaishukuru sana LATRA kwa kutuelewesha faida ya kukata leseni za LATRA kwa sababu ni leseni ambayo tunakata kwa ajili ya kubeba abiria lakini pia tunashukuru maana wametupa elimu ya kwamba tunaweza tukafungua vikundi na kutengeneza ushirika wetu wa bodaboda na tukakata leseni zetu LATRA na kufaidika na asilimia inayotoka LATRA kwaio ikatunufaisha kwa kupata kiasi na kutuinua kiuchumi kwa kupitia mfumo huu” amefafanua Bw. Mgonja

Mchakato wa Uanzishwaji wa Vyama vya ushirika (SACCOS) kwa wamiliki na madereva wa bajaji na bodaboda nchini kote ni mpango wa Mamlaka uliolenga kuwakwamua kiuchumi wanachama wa vyama hivyo huku wakiwa na dhima kubwa ya kujidhibiti wao wenyewe.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo