Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATOA LESENI 334,859 KWA MAGARI YA ABIRIA NA MIZIGO
Imewekwa: 08 May, 2025
LATRA YATOA LESENI 334,859 KWA MAGARI YA ABIRIA NA MIZIGO

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa leseni 334,859 kwa vyombo vya moto kibiashara kuanzia mwaka 2021 hadi Machi 2025 kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (Railway and Road Information Management System - RRIMS) kwa anwani ya https://rrims.latra.go.tz   

amebainisha hayo CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA alipowasilisha mafanikio ya LATRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye semina ya kuwajengea uwezo wanahabari Mabalozi wa LATRA kuhusu uandishi wa habari za LATRA pamoja na kufahamu kazi na majukumu ya Mamlaka, Mei 7, 2025 ukumbi wa TARI uliopo Kibaha Mkoa wa Pwani.

“Idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria (passenger service vehicles), mizigo (goods carrying vehicles), na vyombo vya usafiri wa kukodi (private hire service vehicles) ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 (Februari, 2021) hadi 334,859 mwaka 2024/25 (Machi, 2025), ikiwa ni ongezeko la leseni 108,658, sawa na ongezeko la asilimia 48, Hili ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne (4) inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema CPA Suluo.

Vilevile ameongeza kuwa Mfumo wa RRIMS unamuwezesha Msafirishaji kuchapa leseni yake popote alipo bila kufika ofisi za LATRA na unamwezesha msafirishaji kufanya maombi ya leseni na huduma zake pamoja na kuchapa leseni iliyoidhinishwa ndani ya saa 24 na hivyo kupunguza usumbufu na muda wa kupata huduma.

“RRIMS ni Mfumo mama wa Mamlaka ambao unasaidia katika utoaji wa leseni za magari ya abiria na mizigo, usajili wa madereva, malipo na taarifa za udhibiti na Mfumo huu  umeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za serikali kama vile TRA, TIRA, NIDA, GePG na BRELA ili kurahisisha uhakiki wa leseni zinazotolewa na Mamlaka” amesema CPA Suluo.

Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 kimeipa Mamlaka jukumu la kutoa, kuhuisha, kusitisha na/au kufuta leseni za usafirishaji  magari ya abiria na mizigo ambapo Mfumo wa RRIMS unafanikisha utekelezaji wa jukumu hilo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo