Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATUNUKIWA CHETI NA TAT
Imewekwa: 07 Mar, 2024
LATRA YATUNUKIWA CHETI NA TAT

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amepokea cheti cha kutambua na kuthamini mchango wa Mamlaka katika maendeleo ya sekta ya usafiri nchini kutoka kwa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT). Machi 7, 2024 katika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti hicho, CPA Suluo amesema cheti alichopokea ni kielelezo tosha cha utumishi uliotukuka wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa ndiye aliyeweka mazingira bora, rafiki na wezeshi yaliyochagiza kukua na kuboreshwa kwa sekta ya usafiri nchini.

“Anayestahili hili ni Mhe. Rais Samia ambaye aliniteua ili nimsaidie kusimamia sekta hii. Niwaombe muendelee kuchapa kazi kwa bidii kwa kuwa ndio njia pekee ya kumshukuru kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya kwa wananchi na Taifa kwa jumla,” ameeleza CPA Suluo.

Vilevile amesema kuwa, Serikali inatambua na inathamini kazi kubwa inayofanywa na TAT na vyama vingine vya wasafirishaji na pia inatambua mchango wao katika uchumi wa nchi, na Mamlaka itaendelea kushirikiana nao katika kila hatua ili kufikia malengo na maono ya Mhe. Rais Samia ya kuifanya sekta ya usafiri kuwa bora zaidi.

Pia ameeleza kuwa, cheti hicho kimeipa Mamlaka changamoto zaidi ya kuongeza umakini na ufanisi wakati wa kutekeleza majukumu ya kiudhibiti.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa TAT, Bw. Omar Kiponza, Makamu wa Rais TAT amesema kuwa, wao kama wadau wa usafirishaji nchini, wanatambua juhudi na kazi kubwa inayofanywa na LATRA katika kuhakikisha sekta ya usafiri ardhini inakuwa bora na salama.

Aidha, Bw. Kiponza amempongeza CPA Suluo na uongozi wa Mamlaka kwa kusimamia sekta ya usafiri ardhini kwa weledi na ufanisi, pia kwa kuwa wasikivu na kutatua changamoto zao kwa wakati.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo