Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWANOA WANAHABARI
Imewekwa: 02 Mar, 2024
LATRA YAWANOA WANAHABARI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewaasa wanahabari kutumia kalamu zao vizuri ili kuleta mabadiliko katika jamii kwani Mamlaka inaamini nguvu ya kalamu zao inaweza kusaidia kujenga Taifa linalozingatia utu, uadilifu amani na utulivu.

Hayo yamesemwa na Wakili Tumaini Silaa, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya LATRA wakati akifungua semina ya siku mbili ili kuwajengea uwezo Wanahabari Mabalozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhusu kazi na majukumu ya LATRA katika ukumbi wa hoteli ya Njuweni - Kibaha Mkoani Pwani kuanzia Februari 26 hadi 27, 2024.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Wakili Silaa amewasihi mabalozi hao kuzingatia uzalendo katika utendaji wa kazi zao pamoja na kuzingatia maadili kwani kufanya hivyo kutaleta maendeleo chanya kwa taifa na sekta ya usafiri kwa jumla.

“Tunatambua umuhimu wenu wa kazi kubwa mnayofanya kwa LATRA na kwa nchi hii, vilevile tunatambua mchango mkubwa ambao mmeufanya kwetu katika kuhabarisha na kutoa elimu kwa umma kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na Mamlaka, niwasihi muendelee kufanya kazi kwa kutanguliza uzalendo mbele kwa sababu na nyinyi pia mnaishi katika nchi hii, na mzitumie vyema kalamu zenu katika kuuhabarisha umma,” amesema Wakili Silaa.

Kwa upande wake CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amewapongeza wanahabari mabalozi hao kwa kuhudhuria semina hiyo pamoja kuwa ni mara ya kwanza LATRA  kuandaa semina kama hiyo na kuongeza kuwa LATRA inathamini sana kazi yao ya kuhabarisha jamii kuhusiana na majukumu mbalimbali ya Mamlaka.

“Niwashukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria semina hii, naamini mahali ambapo wanahabari wapo wananchi huwakilishwa vyema, ni matarajio yetu kuwa uwepo wenu hapa utawezesha kujifunza na kuufikishia umma wa watanzania taarifa sahihi kuhusu juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia LATRA ili kujenga Taifa bora lenye kuchapa kazi kwa weledi, amani, utulivu, umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watanzania,” amesema CPA Suluo.

Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, mafanikio ambayo LATRA imeyapata ni kutokana na juhudhi za makusudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia kwa kuijengea LATRA mazingira bora na mazuri katika kusimamia sekta ya usafiri ardhini kwa weledi na ufanisi mkubwa.

“Natumia fursa hii kutoa Pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wenye mafanikio mengi makubwa katika Awamu hii ya Sita. Kwa uchache niseme uongozi wa Mhe. Dkt Samia umetujengea mazingira mazuri, bora na rafiki ya kusimamia sekta ya usafiri ardhini kwa weledi na ufanisi mkubwa tukizingatia sana ushirikishwaji wa wadau wetu wote muhimu” amesema CPA Suluo.

Naye Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara amewaasa mabalozi hao wa habari kushirikiana kuelimisha umma kuhusu haki na wajibu wao watumiapo vyombo vya moto kibiashara pamoja na kuzitolea taarifa changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi kwa LATRA kwani kufanya hivyo italeta tija katika kuboresha sekta ya Usafiri Ardhini.

Kwa upande wake Bi. Helen Nachilongo, mwandishi wa gazeti la The Citizen ameishukuru LATRA kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika semina ya kuwajengea uwezo na kuiomba Mamlaka iendelee na utaratibu huo wa kuwapatia mafunzo kwani imeweka alama kubwa kwao.

Naye Bw. Saidi Mohammed, mwandishi wa Clouds FM amewasihi mabalozi wenzake kuwanufaisha wananchi kwa kile walichokipata kutoka LATRA kwani ni jukumu lao kama waandishi,

Wataalamu wa LATRA waliwasilisha mada mbalimbali kwenye semina hiyo ikiwemo Kanuni Mpya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024 zinazosimamia matumizi ya mfumo wa Tiketi Mtandao, Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari, Kanuni za Uwezeshaji wa Watoa Huduma za Usafirishaji, kanuni za Utaratibu wa Kushughulikia Malalamiko, Udhibiti wa Nauli za vyombo vya Moto Kibiashara na masuala mengine mbalimbali yanayohusu Mamlaka na sekta ya usafiri ardhini kwa jumla

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo