Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWAONYA MADEREVA TEKSI MTANDAO
Imewekwa: 19 Jan, 2023
LATRA YAWAONYA MADEREVA TEKSI MTANDAO

Na Mambwana Jumbe

Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara Bw. Johansen Kahatano amewaonya madereva wa teksi mtandao wanaotoza nauli tofauti na zilizoaidhinishwa na Mamlaka.

Onyo hilo limetolewa kufuatia malalamiko ya baadhi ya abiria wa teksi mtandao ambao wamekutana na kadhia ya kuzidishiwa nauli pindi wanapotumia usafiri huo. Aidha, amewataka abiria wa teksi mtandao kutoa taarifa kwa Mamlaka wanapokutana na changamoto hizo kwa kupiga namba bure 0800110019 inayopatikana saa 24.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema wiki hii katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Kahatano amesema kuwa viwango vya nauli vilivyopangwa na Mamlaka kwa kilometa moja ni kati ya shilingi 800 hadi 1000 na kwa dakika moja ni kati ya shilingi 80 hadi 100 kwa sababu mfumo unaangalia umbali pamoja na muda unaotumika kwenye safari.

“Tunatoa rai kwa wadau wetu wanaotumia teksi mtandao wakiona kuna tofauti yoyote ile watoe taarifa kwa Mamlaka hasa kwa kupiga simu na kutupatia taarifa ya namba ya gari na namba ya simu ya dereva ambaye amemhudumia.  Mamlaka itachunguza usahihi wa taarifa na kuchukua hatua,” amesema Bw. Kahatano.

Vilevile Bw. Kahatano ameongeza kuwa, Mamlaka itafanya uchunguzi wa taarifa hizo na endapo itathibitika kuwa wapo wanaofanya vitendo hivyo, hatua zitachukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wahusika kwenye huduma hiyo.

Akijibu hoja ya madai ya madereva wa teksi mtandao kutozwa makato makubwa na makampuni yanayotoa huduma za teksi mtandao hali ambayo inawasababisha kutoza nauli zaidi ya iliyoidhinishwa na Mamlaka, Bw. Kahatano amesema wanachokifanya ni uhalifu kama uhalifu mwingine, “Hakuna kitu ambacho kinaweza kuhalalisha mtu kuchukua mali ya mtu mwingine bila ridhaa yake. Kwa hiyo kama wao wanaona kwamba hivi viwango ambavyo vimewekwa au makato ni makubwa sana Mamlaka ipo, warudi kwetu tutawasikiliza na ikibidi kufanya mapitio.”

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo